Mrembo Ngangari (Riwaya ya Vita, 18+)



Vumbi jekundu lilikuwa likitimka huku na kule katika eneo la stand mpya ya Kasulu, kila mtu alificha uso wake ili vumbi hilo lisije kumletea madhara yoyote, lakini watoto walionekana kuifurahia hali hiyo walikimbiakimbia kutaka kudaka makaratasi na mifuko ya nailoni iliyokuwa ikipeperushwa na vumbi hilo, kwao ilikuwa ni mchezo mzuri sana, hawakufikiri hata mara moja kuwa vumbi hilo lingeweza kuwaletea madhara au hata upofu, kwao haikuwa hivyo kwani hawakujali hata kesho ikoje.

Katika moja ya migahawa iliyopo stand hapo palikuwa na vijana watatu walioonekana kubishana kitu fulani na kati yao ilionekana hakuna uelewano, lugha waliotumia ilikuwa si ya hapa ila ni ya nchi jirani. Vijana hao waliovalia kitanashati, suruali zilizokaa vizuri katika matumbo yao walinyanyuka kutoka katika mgahawa huo na kutoka nje kila mtu akiwa na mawazo yake, walipanda magari tofauti ya kuelekea Kigoma mjini na kuondoka eneo lile.

Vumbi bado lilikuwa halijatulia katika eneo hilo na watoto wale walikuwa bado wanacheza wakiwa na furaha kabisa huku wengine wakiwa wameshikilia kaptula zao zisiwadondoke. Wengine wkiendelea kucheza kabumbu wakiwa na ndoto za kuwa wachezaji nyota wa dunia siku moja.
Vumbi lile lilitenganisha dunia zilizokuwa hapo kwa wakati huo kila mmoja hakujua nini kinaendelea upande wa pili.

Magari yaliondoka katika eneo lile kwa nyakati tofauti mengine yakielekea Kahama, mengine Manyovu, mengine Kigoma mjini basi ilimradi kila kitu kiliendelea.
Vumbi lilitulia na hali ikawa tulivu katika eneo hilo lote, watoto wale sasa iliwabidi wabadilishe aina ya mchezo kwani ule wa kwanza haukuwa na vitendea kazi tena.

Isabel, msichana mfupi, kibonge mwenye macho ya kuvutia, mweusi kidogo mwenye kucheka na kila amuonaye akaondoa mtandio wake usoni na kupepesa macho huku na huku na kushuhudia utulivu wa hali ya juu stendi hapo
“Kaka samahani hakuna basi lililokuja hapa?” alimrushia swali kijana mmoja aliyekua akiuza vocha eneo hilo
“Ha! We dada mabasi manne yamekuja na kuondoka ulikuwa wapi? Hukuyaona? Itabidi usubiri bahati nyingine” kijana yule alimjibu Isabel, Isabel alitafakari kidogo imekuwaje hakuyaona mabasi yale, kumbe alipojifunika mtandio ule kuzuia vumbi kausingizi kalimpitia ndiyo maana hakujua hata nini kiliendelea stendi hapo, alitafakari kidogo, akanyanyuka kutoka katika bench lile na kuuendea mgahawa Fulani ili apate chochote na kisha aamue afanye nini.

Aliketi kwenye moja ya viti vya plastiki katika mgahawa huo na kuagiza soda na keki, alipokuwa akiendelea kunywa soda yake alihisi kama amekalia kitu Fulani lakini alipuuzia, baada ya muda alipitisha mkono wake kitini alipokaa na kushika kitu Fulani kisha akakitoa ili ajue ni kitu gani “mh” aliguna, alijikuta na bahasha ndogo mkononi ndani ina kitu kigumugumu hivi, baada ya kutazama uku na huku hakuna aliyemuona aliitia bahasha ile katika mkoba wake wa laptop na kumalizia soda yake. Alitoka na kupanda Toyota hiace kuelekea mjini, akiwa ndani ya daladala ile alikuwa na mawazo mengi sana, lengo lake la kurudi ni kuangalia kama kuna treni ya Dar maana mabasi yamempita kwa kuendekeza usingizi.

Josephat Msengiyumva alivua mawani yake ya jua na kuchukua kitambaa kujifuta vumbi kidogo machoni, akiwa amejiegemeza kwenye nguzo ya umeme akiangalia mapito ya wapita njia mfuko wake wa shati ulitikisika kidogo, akaingiza mkono na kutoa simu kuna meseji ilifika muda si mrefu ‘Mr Jomse unayo ile memory card?’ Jomse alistuka kidogo, akili iliporudi aliijibu meseji ile kuwa hana hiyo memory card. Kichwa kilimzunguka na hakujua kama swali aliloulizwa lilikuwa la mzaa au la ‘mzaa katika kazi’ alijiwazia akicheka kidogo kisha akarudisha simu sehemu yake. Mara meseji ikaingia tena ‘na jamaa anasema hana, hapa na mi sina’ . Jomse alishusha pumzi ndefu na kujiondoa pale aliposimama, akasogea pembeni pasipo na watu na kupiga simu “mbona siwaelewi nyi jamaa, kwani wa mwisho kuwa nayo nani?” Jomse aliuliza kwa ukali na baada ya kusubiri sekunde kadhaa aliendelea “ nasema hivi! Mrudi palepale kwenye mgahawa mkaangalie, msilete ujinga unafikiri mama akijua tutasema nini!? Haya nasubiri jibu!” aliwakaripia wenzake na kukata simu kwa hasira na kuirudisha mfukoni.
Jomse alijishika kichwa kuonesha amechoka ghafla.

Memory card ndogo iliyotiwa kwenye kibahasha cheupe ilianza kuwachanganya akili vijana wale, hawakujua wafanye nini, kazi waliyopewa, maelekezo na picha zote zipo ndani ya card hiyo, shughuli pevu.

Mathias Ndirikumana au Mandi kama anavyojulikana kikazi alikuwa wa kwanza kufika katika mgahawa ule, alipoingia moja kwamoja alitupa jicho sehemu mbalimbali za kibanda hiko kwa ufundi sana lakini hakuona dalili ya kibahasha kile
“dada, tulipoondoka hukuona kitu chochote hapa?” alimtupia swali mama lishe yule “hapana kaka, ni kitu gain?” mama lishe alijibu na kuuliza kwa wakati mmoja
“aaah, tumesahau bahasha na hapa tulikuwa nayo, kama umeiona niambie hata pesa nitakupatia” Mandi alimueleza yule mama ntilie ambaye alionesha wazi kuwa kitu hiko hajakiona hata kidogo. Mandi alionesha uso wa kuchanganyikiwa kila wakati alikuwa akijifuta jasho usoni, mara ashike kiuno, mara atikise kichwa.
“Vipi umeipata?” sauti ilitokea nyuma yake, alipogeuka alikutana macho kwa macho na Tonton ambaye alifika mahali hapo muda huo
“hapana Ton, sijaiona” alimjibu
“ah! Huyu dada anasemaje?” Ton aliuliza
“anasema hajaiona kabisa” Mandi alimjibu Tonton, Tonton alishikwa na hasira nakuanza kumfuata yule dada lakini alizuiliwa na mkono wenye nguvu wa Mandi
“tulia Tonton, mbona una pupa” mandi alimtuliza Ton, na Ton alitulia na kuketi kwenye moja ya viti vilivyopo mgahawani hapo.
“Dada! Unakumbuka mi nilikaa hapo kwenye kiti cha pepsi, nilipotoka nani alikaa?” Ton aliuliza, kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa na bahasha hiyo mfukoni.
“Hapo alikaa mdada mmoja hivi, naye ameshaondoka na hiace kwenda mjini, lakini sijui kama yeye kaichukua” mama lishe alimjibu Ton, Mandi na Ton walitazamana kisha wote wakageuka kwa dada yule kabla hawajaongea lolote sauti ya mtoto iliwakatiza
“mama! Kwani hawa wanataka nini?” mtoto yule alimuuliza mama yake,
“wanatafuta bahasha wameipoteza” dada yule alimjibu mtoto huku akimsukuma akacheze “ah! Mi najua, alishika yule dada aliyekaa hapa, hapa kwenye hiki kiti” mtoto alieleza na kisha kukimbia kuendelea kucheza mpira na wenzake.

“Dada huyo msichana alikaa hapa yukoje?” Ton alidakiza swali kwa dada yule.
“Alikuwa amevaa suruali ya jeans nyeusi na tshirt nyekundu, ila sikumbuki ilikuwa imeandikwa nini ana begi jeusi la mgongoni” mama lishe aliwajibu vijana wale, bila kuchelewa Mandi na Ton waliondoka kituoni hapo na kukodi tax
“Kigoma mjini tafadhali” Mandi alimueleza dreva tax huku akifunga mlango na kujiweka vizuri katika kiti cha nyuma. Ton alichukua simu yake na kutuma sms kwa Jomse kumueleza juu ya tukio hilo “sasa tufanyeje?” Jomse alirudisha sms ile kwa Ton, “nafikiri tujaribu kumtrace ikiwezekana

kumpata tuchukue hiyo memory card” . Wazo lilikubaliwa na wote watatu na moja kwa moja Jomse ambaye wakati huo alikuwa mjini moja kwa moja alielekea kituo cha mabasi cha Mwanga ili kujaribu kama anaweza kumpa msichana yule na jinsi gain ya kupata memory card ile.

Vurugu za wapiga debe na wabeba mizigo katika kituo hiko cha mabasi zilishamiri mchana ule, wanaoshuka na wanaopanda mabasi walikuwa ni wengi, Jomse alisimama karibu kabisa na kibanda cha simu, kutokana na urefu aliokuwa nao haikuwa vigumu kuwaona wote waliokuwa katika pilikapilika kituoni hapo. ‘Msichana mfupi, kavaa fulana nyekundu na suruali ya jeans nyeusi’ Jomse alijesemea moyoni maneno hayo huku akiangalia kila daladala inayoshusha abiriria katika eneo hilo.
Mandi na Ton nao waliingia katika eneo hilo na kumshukuru dreva tax, Ton alitoa noti nyekundu moja na kumpatia kijana yule kasha wakajichanganya kuanza msako wao.
Jomse alikuwa makini akiwa na gazeti lake mkononi alijifanya akifungua kurasa hii na ile lakini hakuwa akisoma chochote ndani ya gazeti hilo, aliang’aza macho huku na huku kuangalia kama atamuona msichana yule, huku akili yake ikizidi kuchanganyikiwa juu ya upotevu huo wa memory card, wasiwasi wake ulikuwa ni jinsi gain wataonekana wazembe kwa sababu hata kazi waliyopewa bado hawajaanza kuifanya memory card hiyo wameshaipoteza, Jomse alijua wazi kuwa Mama akisikia jambo hilo watapata shida sana kwani wataonekena wazembe kupita maelezo.
Mandi na Ton waligawana kila mtu upande wake ili wote waweze kuona kama watampata msichana huyo, walikuwa na wasiwasi na daladala waliyoipita njiani, walijua hakika atakuwa katika hiyo, na walipanga watafanya kila hila wampate ili wapate watakacho. Toyota Hiace ya buluu iliingia kituoni hapo na kutafuta maegesho ili ishushe abiria wake, watu walikuwa wengi ndani ya gari hiyo na walianza kushuka mmoja mmoja, “muwe makini katika kufanya hili” sms iliingia katika simu ya Mandi na Tom kwa wakati mmoja “msitumie nguvu ila akili ndiyo inahitajika” sms nyingine iliingia kwa wote wawili.
Isabel alijisikia baridi kidogo akafungua begi lake na kutoa sweta aina ya ‘kaba shingo’ na kulivaa kabla hajashuka katika gari ile, alipohakikisha limemkaa vizuri, taratibu alishuka garini nakuangalia huku na huku kisha kujichanganya na watu wengine kituoni hapo. Msichana anayekadiriwa umri wa miaka kumi nane alishuka katika daladala upande wa pili, Jomse alimgundua haraka msichana yule aliyevalia sweta jekundu na sketi nyeusi, Jomse alimkazia macho lakini alijiuliza kwa nini maelekezo aliyopewa hayakulingana na mtu mwenyewe alivyo, alimtupia jicho mara nyingine na kutoa simu yake mfukoni akaandika kitu Fulani “kwenye mitumba” meseji ziliingia kwa Mandi na Ton, mara moja walimuona msichana yule lakini wote walishangaa kuona hajavaa suruali kama walivyoelekezwa. Ton alisogea taratibu eneo la muuza mitumba ambapo binti yule alionekana akichagua vibrauz vya hapa na pale, alipomwangalia kwa makini aliona kuwa hilo ni windo tofauti na wanalolitaka, alijaribu kuangalia vizuri huku na huku kama atamuona mwingine lakini eneo lote alikuwa ni binti yule tu aliyevaa vile. “Ni huyu kweli?” Ton aliwatumia meseji Jomse na Mandi, hapo nao wakapata shaka wasije kubana mtu tofauti, waliumiza vichwa wafanyeje kwa hilo. Lakini katika eneo hilo hakukuwa na msichana yoyote aliyevaa vile walivyoelekezwa.
Baada ya kuchagua vibrauz viwili yule msichana alinunua mfuko wa Rambo na kuweka kasha akachukua begi la mdogo wake na kuingiza humo na kulitia mgongoni safari ikaendelea. Mandi alimfuata nyuma nyuma msichana yule huku akilipigia taiming begi lile, mpango ulipangwa kiufundi sana. Mara ghafla gari aina ya Toyota mark II ilifunga breki karibu kabisa na msichana yule, Jomse alichomoza na kumvutia ndani kwa haraka kabla hatahamaki gari ile iliondoka kwa kasi. Mandi aliangalia gari ile ilivyotokomea, watu walikusanyana eneo lile kuangalia kilichotokea akina mama wakipiga kelele za msaada
“dada!!, dada!!” mtoto mmoja wa kiume alikuwa akilia kwa uchungu pembeni mwa barabara.

Isabel akiwa na begi lake mgongoni aliona tukio lote lilivyotokea, alipigwa na bumbuwazi alibaki kajishika mdomo, naye alijichanganya na watu wengine katika eneo hilo. Mandi alimtazama Isabel kwa makini kana kwamba kuna sehemu ambayo amekwishawahi kumuona, Isabel alipogeuka alikutana macho kwa macho na Mandi lakini hakumtilia maanani akijua tu ni moja ya wapita njia,
Mandi alimwita Isabel
“we dada njoo umsaidie mtoto huyu” Isabel alikwenda na kumchukua mtoto yule aliyekuwa akilia sana, Isabel aliivuta sweta yake kwa juu na kumfuta machozi mtoto yule, Mandi akiwa bado hajaondoka eneo lile alimuona Isabel alipofanya jambo hilo na mara moja aliiona fulana ile nyekundu iliyotokeza kwa chini baada ya kulivuta sweta lile kwa juu, na lipomwangalia vizuri alimuona kweli kava jeans nyeusi, Mandi alipagawa alitoa simu yake mfukoni na kutuma meseji “Wrong number, rudi haraka namba sahihi umeiacha”, alirudisha simu mfukoni na kuanza kumfuatilia Isabel. Isabel alimkabidhi mtoto yule kwa askari polisi mmoja wa kike ambaye alifika eneo hilo na yeye kuendeea na safari yake.

Mandi alikuwa bado akimwangalia Isabel wapi anakoelekea, Isabel aliangalia saa yake ya mkononi na kuona muda unamuacha alisimamisha bodaboda na kupanda kasha akampa maelekezo Fulani dereva. Mandi naye akachukua bodaboda iliyofuata ile nyingine
“hakikisha hakupotei” Mandi alimsisitiza muendesha bodaboda. Isabel akiwa hajui kama anafuatiliwa alikuwa anawaza tu kama ataiwahi treni ambayo ilikuwa iondoke jioni hiyo kuelekea Tabora mpaka Dar huku akiwa ameshasahau juu ya ile bahasha. Simulizi hii ni ya kivita au kijasusi hasa yaani matumizi ya  nguvu, silaha na mapigano ya aina mbalimbali na mapenzi kiasi, Whatsapp/Call +255 758 018 597 Email – kulayagroup@gmail.com

Post a Comment

0 Comments