KAMANDA Amata alikuwa kachanganyikiwa akili kwa namna moja au
nyingine, alikuwa akiona kama ndoto inayotokea mbele yake, hakuamini kama
wamewahiwa namna hiyo na kwa kasi ya ajabu, alijiuliza kila wakati ni nani
mwenye uwezo wa kuwanasa namna hiyo, hakupata jibu zaidi ya hapo aligundua kuwa
kwa vyovyote ni watu hatari wanaojua nini wanafanya na kwa wakati pia alielewa
watu hao wamepewa kazi kwa muda maalumu hivyo na yeye kama ilimpasa kuwa saidia
wenzake alitakiwa ajipe muda maalum na muda wa kazi yake uwe mdogo kuiko muda
wa adui zake pia ucheze ndani ya muda wa adui zake. Alitikisa kichwa kana
kwamba kuna mdudu akimtembea kwenye ubongo wake, akaitazama saa yake, saa
zinayoyoma kwelikweli.
Ilikuwa inakaribia saa nane usiku alipokuwa akifungua geti la
nyumbani kwake, akaingia na kulifunga nyuma yake, kisha akasimama kidogo
kuangalia nini kinaendelea huku na kule, kwa macho yake makali aliweza kuona ua
moja kubwa likitikisika kidogo, akaelewa wazi kuwa mtikiso huo lazima kuna kitu
na si wa upepo kwani hali ya hewe ilikuwa imetulia sana na haikuwa na upepo.
Damu ikamtembe haraka mwilini, hakufanya lolote, akauendea mlango wa nyumba
kubwa na alipoufikia alikuta karatasi iliyoning’inizwa mlangoni, kisu chembamba
chenye makali kuwili kilitumika kuishikia hiyo karatasi pale mlango.
Mwisho wa zama zenu umefika, mtaongea na Ngurumo.
Ulikuwa ujumbe uliosomeka katika karatasi hiyo pale juu.
Akakikamata kile kisu na kukichomoa kwa nguvu, akakibusu, akaiokota ile
karatasi na kuishika mkononi kisha akaingia ndani na kuuacha mlango wa nyumba
yake bila kuufunga makusudi tu. Moja kwa moja akakiendea chumba chake na
kufungua kabati kubwa lililokuwa mbele yake. Akavuta fulana yake nyeusi kaba
shingo ya mikono mirefu akaivaa ikitanguliwa na vesti nyeusi pia. Kizibao
cheusi chenye mifuko mingi ya kuwekea zana mbalimbali kikafuata juu yake, na
zana zake zikapachikwa, bastola nne zilizosheheni risasi zikakaa mahala pake,
visu vidogodogo vikawekwa mahala pake, paketi za risasi zikawekwa mahala pake,
Shotgun mbili zikabanwa mahala pake nazo zikiwa zimetimia. Akakusanya
vikolokolo vya kutosha kwa pambano hilo ambalo hakujua ni nani haswa anakwenda
kupambana naye.
Akiwa kasimama kwenye kioo, anajiweka sawa, akahisi vinyweleo
vyake vikisimama, mwili ukamsisimka, akajua kuna jambo, akalisubiri huku
akijifanya hajui lolote.
Palepale kwenye kioo alimuona mtu akiingia kwa minyato kumfuata,
Kamanda alitamani kucheka kwa sababu hata kama alikuwa akinyata wakati yeye
alikuwa akimuona kwenye kioo ni kazi bure. Akamsubiri amkaribie ili ajue nini
cha kumfanya. Yule mtu akajiandaa kwa waya aliokuwa kaufunga kutoka mkono hu
mpaka ule mwingine.
Anataka kunikaba, Kamanda akawaza. Kisha kwa kasi ya ajabu
akageuka na guu lake lenye nguvu likatua kichwani mwa Yule mtu, akajibwaga na
kujibamiza kwenye mwamba wa kitanda, yowe la maumivu likamtoka, kabla hajafanya
lolote akamnyanyua na kumpa kichapo kikali, alipohakikisha kuwa hali aliyokuwa
nayo hawezi fanya lolote akamkalisha chini na kumwegemeza ukutani, akamtikisa
na kumtazama usoni.
“Nani bosi wako?” akamwuliza.
“Si-si-simjui!” akajibu kwa tabu.
“Unaniletea utani siyo?” akamwuliza kwa ukali.
“Kweli simjui, mi natumwa tu na kulipwa ujira mkubwa wa
kunitosha, kwa hali ya nchi yetu nakubali kufanya kazi yoyote kwa malipo
yoyote,” akajieleza.
“Nafikiri hunijui sawa sawa sasa utanijua!” Kamanda akamwambia
kisha akamkamata korodani zake na kuziminya kwa nguvu.
“Aaaaaiiiiggggghhhh…. Niache, niache nitasema,” akalia kwa
uchungu.
“Sema, nani bosi wako, nani aliyekutuma kuja hapa?” kamanda
akauliza sasa kwa ukali zaidi.
“Kweli kaka sim-ju-jui…” akajibu huku akijigeuza geuza.
Kabla Kamanda hajauliza linguine, akashuhudia povu jeupe
likitoka kinywani mwa Yule mtu.
“Shiiit! Limejiua,” akang’aka kwa sauti, akaanza kumpekua.
Katika moja ya mfuko wa suruali yake akatoa simu ya mkononi,
zaidi ya hapo hakuona chochote cha maana. Akaitazama ile simu, akaenda kwenye
kitabu cha majina akakuta majina matano tu, la kwanza kabisa likamvutia,
lilikuwa limeandikwa kwa jina moja tu ‘Naima’, kisha akaliangalia la
pili na la tatu. Akaamua kuanza kampeni na jina hilo la kwanza.
Akaperuzi upande wa ujumbe mfupi, akakutana na ujumbe kutoka kwa
Naima uliotumwa ndani ya dakika kumi zilizopita lakini ulionekana kutojibiwa.
‘…Akifika nijulishe nije nimalize kazi…’ ujumbe ulisema hivyo.
Lilifikiri litaniweza, sasa naanza na Naima, kawaza na kuamua
kuujibu ule ujumbe.
Kamanda Amata akaujibu ule ujumbe, kisha akaburuza mwili wa Yule
mtu na kuubwaga katika mlango wan je kisha yeye akalitoa pikipiki lake na
kuliegesha nje kabisa, akisubiri kuona kinachoendelea.
Akiwa nje ya nyumba yake, juu yapikipiki lake kubwa akasubiri
kimya nje kabisa ya nyumba yake.
Dakika tano hazikupita, mwanga wa taa za gari ukaonekana
ukijitokeza katika kona ya barabara na kuelekea mtaa huo ilipo nyumba ya
Kamanda Amata. Ilikuwa Ford Ranger nyeusi, haikuwa na namba za usajili, ikasoge
polepole na kuegeshwa karibu kabisa na lango la nyumba hiyo, watu watatu
wakashuka, mmoja kati yao alikuwa mwanamke, alionekana ndiye akiongoza wengine,
aliwapanga, mmoja alimwamuru abaki langoni, yeye na mwingine aliyeonekana pande
la jitu waliingia ndani.
§§§§§
Naima na lile jitu moja kwa moja waliingia getini na kutembea
kwa minyato huku silaha zikiwa mikononi mwao. Wakiwa wanajigawa kiufundi zaidi
kuuelekea mlango, walishangazwa na ukimya uliotawala, lakini hawakujali.
Lilikuwa ni lile pande la mtu lililotangulia kuuendea mlango, kabla halijafika
likajikwaa kwenye kitu kama gogo.
“Aah!” likajivuta na kujibwaga mbele. Lilipogeuka nyuma likaona
mwili wa binadamu, “Shiit! Amemuua,” akasema kwa sauti.
“Nani amemuua?” Naima akauliza, kisha akashusha silaha yake na
kusogea pale ulipo ule mwili, akaugeuza, na kuchomoa kijikaratasi
kilichopachikwa kinywani mwa marehemu.
…Naanza na wewe…
Naima akageuka huku na kule asione mtu, anaanza na mimi!
Hata kama Naima alikuwa ni muuaji mzuri kitaaluma lakini alijikuta akishikwa na
ubaridi wa ghafla. Wakaingia ndani wakatafuta huku na kule hawakuona mtu zaidi
ya redio kubwa iliyokuwa ikipiga muziki laini wa ‘Killing me softly’ akasonya
na kutoka nje. Wakabeba mwili wa mwenzao na kutoka nao.Wakaubwaga katika nyuma
ya pikap yao na kufungia. Kisha nao wakaingia garini na kuondoka.
§§§§§§
Kamanda Amata akawasha pikipiki lake, bila kuwasha taa, akaingia
barabarani na kuwafuata taratibu, wakaikamata barabara ya Kinondoni na kuvuka
daraja la Salenda kisha wakaelekea mjini, moja kwa moja mpaka Mbowe Club,
wakaegesha gari na kuteremka kisha wakapotelea ndani.
Kamanda Amata akaingia baada yao na kuhakikisha hawapotezi
katika himaya ya macho yake, akaketi katika moja ya viti vya kaunta na kuagiza
glass moja ya Whisky akachanganya na sprite baridi kisha akawa anakunywa
taratibu.
Wale jamaa wakaketi mahala Fulani wakijadiliana jambo lakini
wakionekana kuwa na wasiwasi, kila mara Naima alionekana kuisoma ile karatasi
na kuiweka tena mfukoni. Mara lile jitu la miraba mine likanyanyuka na kutoka
mahala pale likamwacha Naima na mwingine mmoja. Kamanda Amata alipogeuka
hakuliona lile jitu limeingilia kona gani, akili yake ikazunguka mara mbili,
akateremka katika kile kiti na kujichanganya katikati ya watu waliokuwa
wakiburudika na uziki katika ukumbi huo. Dakika kadhaa baadae akaliona lile
jitu pale kaunta likinga’aang’aa macho, likabeba vinywaji na kuelekea kule
lilikokaa tangu mwanzo, yote hayo Kamanda Amata alikuwa akiyatazama kutoka
katika kundi la watu wale. Alipoona kuwa hakuna aliye na yeye alirudi tena
kaunta na kuagiza kinywaji, lakini hakuweza kukimaliza baada ya kumwona Naima
akinyanyuka kitini na kuelekea nje, Kamanda Amata naye akatoka na kumfuatilia
mwanadada huyo.
Naima alisimama kati ya magari na kuweka simu yake sikioni kisha
akaendelea kuongea na aliyekuwa upande wa pili.
Naima akiwa anaendelea kuongea na simu alihisi ubaridi ukimgusa
maeneo ya shingoni, akashtuka akataka kugeuka.
“Tulia!” sauti nzito ya Kamanda Amata ikapenya sikioni mwake.
Naima akatulia kama alivyoamuriwa, “Nilikwambia nitaanza na wewe, na ndiyo sasa
naanza,” akaongeza.
“Weweni nani?” Naima akauliza kwa sauti yake nyororo inayoweza
kumnyong’onyesha mwanaume yeyote Yule rijali.
“Mimi ni Yule mnayenitafuta, Kamanda Amata, na nataka unambie
watu wangu wako wapi?” Kamanda akaongeza swali kisha akatulia. Naima naye
alitulia bila kujibu, akitafakari la kufanya. Baada ya sekunde kadhaa, uamuzi
aliofuanya haukuwa mzuri hata kidogo. Aligeuka na pigo kali kwa Kamanda Amata,
lakini Kamanda aliliepa kiufundi huku bastola yake ikimtoka mikononi. Naima
aliruka sarakasi kwa minajiri ya kuiwahi le bastola lakini kabla hajafika
alijikuta akipokea teka la nguvu mbavuni na kutupwa upande wa pili, akajiinua
haraka na kusimama wima kumkabili Amata. Amata alijiweka sawa mwili wake na kumwendea
kama mbogo, Naima alijiweka sawa na kuvamiana na Amata, kama Kamanda alifikiri
mwanamke huyo anapigika kirahisi alikosea, mapigo matatu ya haraka yalimwingia
Kamanda akajikuta anapoteza netweki, akajaribu kujitutumua lakini akajikuta
amedhibitiwa ka mikono imara ya mwanamama huyo.
Naima alijirusha hewani kama jani la mkorosho na kuachia dabo
kiki za maana zilizotua sawia kifuani mwake na kumpeleka chini.
Kisha Naima akatua chini kwa miguu miwilia akimtazama Kamanda
Amata akigalagala chini.
“Ha ha ha ha niliambiwa kuwa Amata ni mwanamume wa chuma kaa
mbali naye! Chuma kiko wapi hapa? Na sasa nakuua kwa mkono wangu kwani
nimeahidiwa pesa nyingi sana kama roho yako nikiipeleka kwa bosi wangu,” Naima
aliongea kwa kujiamini huku akiiweka sawa mikono yake tayari kumshushia pigo la
mwisho kijana huyo. Alipomjia kumvamia alimshuhudia Kamanda Amata akijirusha
kutoka chini kwa mtindo wa ajabu na guu lake la kulia likatua chini ya kidevu
cha Naima, akanyanyuliwa na kubwagwa upande wa pili meno kadhaa yakimtoka.
“Mpo chini ya ulinzi!” sauti kali ikasikika upande mwingine.
Kamanda alipotupa jicho akaona polisi eneo hilo, akaruka sarakasi na kutua
upande wa pili wa gari, akajibana sehemu ambayo kutokana na nguo zake hakuweza
kuonekana, akitazama linaloendelea.
Amata alishuhudia wale polisi wawili wakichezea kichapo….
Whatsapp +255 758 018 597
0 Comments
Karibu sana, tuma ujumbe whatsapp +255 758 018 597 kujipatia simulizi zetu
Emoji