Jinini Tikiso (Riwaya) - Fantansia

Jina langu naitwa Vegasi Mbwana marafiki walipenda kuniita Vega, ni mzaliwa wa Kigoma Ujiji, nina miaka thelathini na tatu ni baba wa watoto wawili Hussein na Khadija, japo ni mwenyeji wa Kigoma ila kwa sasa naishi Jijini Dar wilaya ya Kinondoni eneo moja linaitwa Mwananyamala komakoma huko naishi mimi, mke wangu Latifa Binti Kassim Bakari pamoja na wanetu wawili.
Nilikuwa natoka katika familia yenye maisha ya kati yaani si maisha ya kimasikini wala siyo maisha ya kitajiri, mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne nikiwa ni mwanamume pekee wadogo zangu wote wakiwa ni wasichana naweza nikasema mimi ndio nilikuwa tegemeo kubwa la familia siku za usoni.
Nikililifahamu jambo hilo ilikuwa ni moja ya motisha kukazana katika masomo yangu nikielewa mimi ndio tegemeo la familia.
Juhudi zangu katika masomo zilinifanya niwe miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakitazamwa na uongozi wa shule hata wanafunzi wenzangu pia, kama miongoni mwa watu watakao faulu bila zengwe.
Uwezo mzuri kitaaluma ulinipatia marafiki wengi ukichangia na ule ukarimu wangu ukiachilia mbali kipaji changu cha usakataji kabumbu kipaji kilicho niongezea umaarufu mkubwa kabisa kila kona ya mji wa Kigoma.
Mfanano wa majina kati yangu na mchezaji mahili wa klabu ya Liverpool ya nchini Wingereza ajulikanaye kama Patric Vegas ilinifanya kuwa mpenzi mkubwa wa mchezaji huyo na kumfanya kuwa role model wangu, hatua iliyo pelekea kuwa mchezaji hatari ninaye chipukia, mwenye ndoto za soka la kimataifa.
Nathubutu kusema nilikuwa maarufu kule Kigoma kuliko hata mkuu wa wilaya ya Kigoma
Fauku ya hayo, masiku kadhaa nilifanya mtihani wangu wa mwisho wa kidato cha sita na kama ilivyo tarajiwa na watu wengi nilikuwa ni moja kati ya wahitimu wa kidato sita wa shule ya sekondari ya Newman, niliye faulu kwa alama za juu kabisa na kubahatika kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salam nikitazamia kuanza masomo ya shahada ya kwanza ya ualimu.
Nakumbuka Ilikuwa ni majira ya saa moja kama na nusu hivi za jioni, mimi na marafiki wachache, tulikuwa katika hafla ndogo katika ukumbi maarufu pale Kigoma, kizota pub, ilikuwa ni sherehe ya kusherehekea ushindi wa timu yetu ya ‘Joy football club’ kupanda daraja na kuwa miongoni mwa timu zitakazo ingia katika ligi kuu ya hapa nchini, ligi iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Ilikuwa ni timu imilikiwayo na shirika moja la watu wa Marekani lijulikanalo kama joy the harvest, shirika ambalo linajihusisha na maendeleo ya jamii kiuchumi, afya na kiroho ambalo lilkuwa chini ya kanisa la katoliki,parokia ya Kigoma Ujiji, ilikuwa ni sherehe ndogo tu iliyo jumuisha wachezaji wa timu, makocha, viongozi wa timu, na mashabiki wachache.

Naikumbuka sana siku hiyo, siku iliyo badili dira nzima ya maisha yangu, siku isiyo weza kufutika akilini mwangu milele na milele, siku iliyo nibadili kutoka katika ubinadamu na kuwa kiumbe wa ajabu kabisa.
Sherehe ilienda mpaka majira ya saa saba usiku kisha hafla ile ikahitimishwa na mgeni rasmi Mheshimiwa Regina Olemunzu huyu ni Afsa ustawi wa jamii wa Manispaa ya mkoa wa Kigoma Ujiji.
Wachezaji wote tulitoka nje ya ukumbi kabla ya kurudishwa kambini ambako tulitakiwa kukaa tena kwa siku moja kabla ya kuvunjwa kwa kambi na askofu mkuu wa mkoa wa Kigoma Father Mathiasi Festo Mberekelwa na watu kurejea majumbani mwao.
Usiku ulikuwa umekuwa mkubwa, giza lilikuwa nene, miale ya radi ilikuwa ikimulika kila baada ya sekunde tano huku ikifuatiwa na ngurumo kali za radi. Dalili ya mvua kubwa ilionekana.
Pamoja na ukweli kwamba siku hii ilifurahiwa na kila mchezaji wa timu yetu hali ilikuwa tofauti kwangu mie!
Sikuwa katika hali ya kawaida na haikuwa wakati ule ambapo nipo ndani ya basi, la! hasha! hali ile ya kutokuwa na raha nilikuwa nayo tangu mwanzo wa sherehe.
Sikuwa ni mwenye furaha kabisa kuna kitu nilikuwa napenda niwe nacho wakati ule lakini ajabu sikujua ni kitu gani.
Kuna wakati katika sherehe niliona kama sherehe ilikuwa ina mapungufu fulani, lakini ungeniuliza ni mapungufu gani bado nisingeweza kuwa na jibu kamili. Kwa lugha ya kueleweka naweza nikasema sikujua nini nahitaji.
‘Nahitaji nini mimi’ nilijuliza akilini huku mawazo yangu yakihamia kwa Nasra, mpenzi mwenye mwenekano wa mwanamke wa urembo.
Lakini wapi. Sikuwa nimemkosa binti huyo japo nilikuwa nampenda mno.
Sasa kumbe nahitaji nini mimi..? niliendelea kujiuliza mwenyewe bila kupata majibu.
Niliishia kuelekeza macho yangu huko nje ambako kulikuwa na giza nene huku anga yote ikimezwa na wingu jeusi la mvua, huku miale ya radi ikimweka kama mwanga wa flashi ya kamera, upepo ikiwa unakusanya takataka nyingi za mtaani na kuzisukuma hovyo kila mahali. Barabarani kukiwa hakuna gari lolote zaidi ya basi letu.
“Yakhee! vipi weye, wajionaje leo, mbona uko hivyo ati?,” nilistushwa na sauti ya Abduli Kareem Babu maarufu kwa jina la Mpemba, mwenyeji wa visiwani Pemba huko Zanzibar, rafiki mchezaji niliyependa kusikia lafudhi ya Kizenji kutoka kwake.
“Unasemaje Mpemba?” nilimuuliza huku nikitabasamu ilhali swali lake nililisikia vema.
“Ati, leo wapatwa na maswahibu gani weye? Mbona huna raha kabisaa? Aliuliza tena, nilijikuta nikitabasamu pasi na kufungua kinywa!
PLAY STORE - SWAHILI SIMULIZI APP
Nikaendelea kupata burudani kwa lafudhi tamu ya lugha adimu ya Kiswahili.
Lakini kabla sijamjibu lolote Mpemba, mara kulitokea kishindo kikubwa kilichofanya watu wote tutoe sauti kali za kuogofya huku hali ya sintofahamu ikichukua hatamu mule ndani ya basi dogo aina ya ya kosta.
Ndani ya nukta chache gari liliacha njia, likawa linaserereka kwa kasi, likijibamiza katika matuta na kuruka juu sentimita kadhaa na kujibamiza tena ardhini, ndani ya gari, kelele za kuogofya za kila aina zilililindima vibaya mno.
Moyo wangu ukalipuka, hofu ikatambaa kifuani mwagu, macho yakanitoka, nikakamatilia kwa nguvu zote mgongo wa siti ya mbele yangu, jasho likiwa linanichuruzika vibaya mno.
“Paaaaaaa” gari lilijibamiza katika tuta huku likizidi kuserereka kwa kasi nilitupa macho mbele kwa dereva nikaona jamaa akiwa anapiga makelele hovyo huku akiwa ameng’ang’ania usukani kwa nguvu.
Sasa tulikuwa katika mteremko mkali kutokea pale Mwanga kwa mchaga kuelekea katika Kituo cha treni Kigoma.
“Ooo! Mungu wangu uko wapi wewe Mungu wewe!..aagh” nilijikuta nikibwabwaja macho yamenitoka, hadi wakati huo yote hayo yanatokea, hakuna aliyekuwa anajua nini chanzo cha yote hayo!
Ingawa akili yangu ikakiri kuwa mwenye majibu ya yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya gari kwa muda huo ni dereva peke yake.
Gari lilienda mrama yule dereva mpiga makelele akiwa ameng’ang’ania usukani kwa nguvu na wakati huo tukawa usawa wa hoteli ya Mwaka Hill.
Eneo lile pembezoni mwa barabara kulikuwa na maporomoko marefu, ambayo licha ya urefu wake pia yalikuwa na upana mkubwa wa mita kama nne ama nne na nusu, ndani ya mtaro huo ambao pia nadhani siyo vizuri nikiuita mtaro labda ni sahihi kusema maporomoko.
Mara nyingi maporomoko hayo yalikuwa yakitumika kwa kutiririshia maji taka kutoka mitaa ya Mji Mwema.
Yule dereva aliyekuwa amepatwa na wazimu wa kupiga makelele hovyo huku mikono yake ikiwa imekamatilia kwa nguvu usukani wa gari, katika hali isiyo ya kawaida alilipeleka gari lile katika maporomoko yale.
“Hehe..hehe..hohooooh, huyu dereva ana wazimu nini,.sasa nini..hii..huku” nilitoa miguno yenye kitetemeshi huku watu wengine pia wakitoa mayowe ya kuogofya. “vuuuuuuu…paaaaaaaa” gari lilitumbukia vibaya na kujibamiza kwa nguvu ndani ya maporoko makubwa ya maji taka!.
Hakuna kilichosalia.
Macho yangu yaligubikwa na giza zito huku maumivu makali yakitambaa kichwani mwangu kwani nilijibamiza vibaya katika vyuma hapo sikujua tena kilichoendelea duniani..
e. Kulaya
“Hii nyumba ya mzee Ramadhani Nswima,. ni nyumba au mti wa mwembe huu!.nyumba gani mvua kidogo inavuja kama tuko nje!.nyumba gani bati lina matundu kibao kama tenga, nyumba wakati wa masika, roho zinakuwa juu juu, anajua kudai kodi tu ila ukarabati wa nyumba hajui..tutahama hapa aagh!..”
“Ta ta ta ta ta” matone ya mvua yalizidi kunidondokea hali iliyozidisha wahka ndani ya roho yangu.. ‘nyumba gani hii sasa!Ona hadi nashindwa kulala aagh”
“Ta ta ta ta” matone ya mvua yaliendelea kunilowanisha.
Sikuweza kuendelea kufumba macho. Kivivu nilifumbua macho yangu hapo maumivu makali kutokea kichwani yalinitambaa mwili wote na ndani ya nusu dakika baada ya kufumbua macho yangu niliona sikuwa chumbani mwangu nilikuwa chini ya kolongo nikiwa nimebanwa na vyuma vya gari lililopolomokea huko chini bondeni.
Mvua kubwa ya mawe na upepo ikiwa inanyesha kwa nguvu.
Hapo kumbukumbu zangu zikarejea upesi kila kitu kilichotokea dakika kadhaa kilipita kichwani mwangu, sasa hii siyo ndoto kama nilivyokuwa nikiota, huu ni ukweli halisi unaoendelea kutokea.
Nilijivuta kwa tabu nikijaribu kujinasua katika vyuma nilivyokuwa nimenasa mule ndani ya gari, maumivu ya kichwa yalizidi kunipa hali ngumu, kichwa kilikuwa kizito kama nimebeba gunia la mchanga.
Lakini hata hivyo kwa tabu nilijtahidi nikajinasua katika uvungu ule wa siti nilipokua nimenasa, gari likiwa limepinduka kimabavu, nikawa natambaa kwa shida kutafuta uwazi wa kutokea nje ya gari.
Katika hangaika ya huku na kule, mara nikapata kuona, tofauti ya kitu ambacho kabla sikuwa nimekifikilia.. ndani ya gari nilikuwa peke yangu, wenzangu hawakuwepo, hata mtu mmoja sikumwona mule garini.
“Weye mpemba weee!” niliita kwa tabu lakini sauti haikufika popote
“Mko wapi ninyi watu” niliendelea kuhaha
Kimya.

“Omariii..” niliita tena kwa sauti ya juu kidogo.
Kimya kingine..
Sikujibiwa na sauti yoyote zaidi ya matone ya mvua yaliyokuwa yakidondoka na mkoromo hafifu wa gari.
Kwa bahati nikafanikiwa kupata uwazi mdogo wa dirisha lililokuwa limepasuka, hapo nikapenya na kutoka nje ya gari.
Bado maumivu mwilini mwangu yalizidi kunitambaa mwili wote na kunipa wakati mgumu mno.
Nilizunguka gari lote pale kolongoni lakini sikuona miili ya wenzangu.
Labda kuna msaada fulani ulipatikana kwa wenzangu wakati mimi nikiwa nimepoteza fahamu chini ya uvungu wa siti ya gari! Lakini ndio wapate msaada waniche peke yangu kule bondeni.
Niliwaza jambo hilo kichwani japo upande wa pili kiudadisi zaidi lilinipa mashaka kidogo, lakini nililazimika kuamini hivyo, yakuwa wenzangu walipata msaada fulani ndiyo maana hakuna ninaemwona eneo lile la tukio
Sasa nikawa nafanya jitihada za kupandisha kule chini ya lile kolongo ambapo nitatokea juu ya barabara huku nikiamini nitapata msaada japo ilikuwa ni usiku mwingi.
Mvua ilizidi kunyesha..
Ulikuwa ni usiku mbaya mno, giza lilikuwa limetanda, macho yangu yaliweza kuona mbele pale mwanga wa radi ulipomweka ngurumo kali za radi zilizidi kuufanya usiku huo uwe wa kuogopesha zaidi, kwa mujibu wa saa yangu ya mkononi ilikuwa ni saa tisa na nusu za usiku.
Sasa nikiwa kule chini ya kolongo nikawa napanda kuelekea juu kwa kushikilia mawe yaliyokuwa pembezoni mwa ukuta, kwa bahati mbaya sikuweza kufanikiwa kufika juu kwani mawe yalikuwa yamelowa na hayakuwa imara kila jiwe nililokuwa nikishika lilikuwa likimomonyoka.
Lakini pia haikuwa kazi rahisi kwani giza nalo lilinipa hali ngumu zaidi, sikuweza kuona wapi nishike na nipite wapi, vilevile si hilo tu hali dhaifu niliyokuwa nayo maumivu yaliyokuwa mwili mzima pia yalinidhoofisha sana.
Sasa nikawa natembea kurudi nyuma kule mwanzo wa maji yanapochuruzikia ni umbali wa mita kama arobaini ndipo kolongo linapoanzia.
Niliamini nikifika mwanzo wa kolongo itakuwa rahisi kutoka kule chini na kupata msaada, kwani kule mwinuko ni wa kawaida na pia eneo lile ni karibu na benki ambapo kwa majira yale, niliamini lazima nitapata msaada hata kutoka kwa walinzi wanaolinda maeneo yale nyakati zile.
Nianza kutembea kwa mwendo wa taratibu na tahadhari kubwa. Mvua iliendelea kunyesha kwa nguvu huku wingu jeusi likiwa limefunika anga na kufanya giza kubwa.
Ilikuwa ni mwendo wa mita kama ishirini na ushee hivi mwanga wa radi ukamulika, kwa sekunde za kuhesabu ikiwa ni kama vile mwanga wa kamera {flash light} mita kama tatu mbele yangu macho yangu yakapata kuona kitu..
Alikuwa ni mtu amelala kifudifudi..lakini sikuwa na uhakika moja kwa moja kama ni mtu.
Radi ikamulika tena, macho yangu yakawa makini zaidi pale mbele, hapo sikupata shaka tena kuelewa ni kitu gani macho yangu yaliona. Alikuwa ni mtu!
Akili yangu ilipata mawenge ghafla, kwani hisia thabiti nilizokuwa nazo kuwa ni lazima yule mtu pale ni miongoni mwa wezangu niliokuwa nao katika basi, sasa vipi tena awe eneo hili, mbali kabisa na eneo la ajali ilipotokea..!

Hii inakuwaje hii..
Hapa lile wazo langu la awali kuwa inawezekana mimi nilisahaulika kuokolewa katika ile ajali na hata kujikuta nipo peke yangu likajirudia kichwani mwangu na nikalifutilia mbali, kwani sikuona mantiki ya fikra hizo kwa sababu mbele yangu kuna mwili wa mtu, ambaye bila shaka ni miongoni mwa wahanga wa ajali ile, japo sikuwa na uhakika wa asilimia zote kuhusu hali yake, nilizipiga hatua kusogea pale ule mwili ulipo.
"Oyaaaa! Ma boy komredi" niliita kwa sauti ya juu kidogo majina ambayo wachezaji wote wa cklabu yetu huwa tunaitana hivyo.
Kimya..
Jamaa alibaki akiwa amelala chali hatikisiki wala hajibu
"Komredi vipi inakuwaje hii..washkaji wengine wapi af..." kabla sijamaliza sentesi yangu.. mwanga wa radi ukaangaza tena..."mamaaaaaaa!!." nilipiga makelele kwa nguvu.
Nilitishika vibaya mno sijawahi kuona kile nilichokiona kabla, kwa zile sekunde tatu za mwanga wa radi zilitosha kunionyesha tukio baya mno, oooh! nilitetemeka, nguvu miguuni zikinitoka, nikajikuta naparamia mawe na kujikwaa kisha nikadondoka chini, midomo ikiwa wazi macho yamenitoka pima, niliogopa mno.
Ulikuwa ni mwili usiyo kuwa na uhai, pili alikuwa ni jamaa yangu Mpemba, rafiki mchezaji, tatu ambalo ndio kubwa ni namna kile nilichokiona kwake kilivyonipa kimuhemuhe, Mpemba alikuwa amepasuka kifua na tumbo huku mapafu, bandama na utumbo vikiwa vinaninging'inia..
Mwili wake ulikuwa umechanwachanwa na kitu chenye ncha kali na kutengeneza majeraha kama ya samaki wa kubanikwa wanavyotayarishwa, usoni alionekana ni mtu aliyekuwa katika taabu ya maumivu makali kabla ya kufa.
Nilijiburuza pale chini macho yangu yakiwa yanakodoa hovyo nahema kwa pupa huku sauti ya kilio nikiifinya kwa chini. nikijitenga mbali na mwili ule wa Mpemba. Hofu kuu ikiwa kifuani mwangu ikanambia, "hii si ajali hii..haya ni mauwaji,.na muuwaji hayuko mbali,” nilipagawa nikiweweseka na kihangaika kugeuka huku na kule.
Yaliyo mkuta mpemba kwa hakika hayakuwa ni matokeo ya ajali bali ni mauwaji ya kukusudia, tena inawezekana muuuwaji alidhamilia kabisa kufanya kitendo kile, na kama hofu yangu ilivyo nambia muuwaji hakuwa mbali eneo lile kwani majeraha yake yalikuwa bado mabichi kabisa.
Vilevile majeraha yale yalinionyesha namna muuwaji alivyo na roho ya kikatili.
Nikawa umbali fulani kutokea pale katika maiti ya mpemba, pembeni kabisa ya ukuta wa jabali, nikawa nimejikunyata kitako miguu nimeivuta sambamba na kifua changu, kamasi jembamba likinitoka huku jasho pia likiwa jingi mwilini mwangu ilihali mvua kubwa ya upepo ilikuwa ikinyesha
"Paaaaa" Sauti kali kama ya bomu ilisikika na kufanya mtikisiko eneo lote.."uwiiiii" nilipiga kelele za hofu huku nikijiziba uso wangu. sasa zamu yangu ya kupasuliwa tumbo na kifua na muuwaji imewadia...
Lakini kumbe ilikuwa ni ngurumo tu ya radi..ilifuatiwa na miale mikali kama umeme na matone ya mvua yakiongeza kasi.. lazma niondoke eneo hili upesi nikatoe taarifa.. nilijiambia moyoni nikajikaza kiume na kusimama wima sasa nikazipiga hatua za kasi huku nikipepesuka kama mlevi lakini ilikuwa ni hatua nne tu ndizo nilizo fanikiwa kuzipiga.
Wakati napiga hatua ya tano ndipo hapo nilipo hisi kuguswa na kitu kama kiganja cha mkono begani mwangu.."ayiiii" nilitoa sauti ya mshtuko nikiruka hatua moja mbele kisha nikageuka nyuma upesi.
Macho kwa macho na kiumbe wa ajabu.
Uwiiiiii,.nakufaaaaa, nilipiga makele punde macho yangu yalipo ona umbo la kiumbe yule.
Alikuwa ni kiumbe nisiye pata kumwona katika huu ulimwengu popo si popo, binadamu si binadamu wala nyani si nyani, lilikuwa ni jitu la miraba minne, lenye kiwili wili kama cha binadamu huku nyuma ya mgongo wake kukiwa na mabawa kama ya popo, kichwa na uso wake ulikuwa kama sokwe mzee, huku mwili mzima ukiwa na manyoya lukuki, hakuwa na nguo isipo kuwa mwili wake wote ulizingilwa na manyoya..'JINI' ndio sifa pekee iliyo penyeza kichwani mwangu kwani ni majini ndio nimewahi kusikia na kusoma katika baaadhi ya vitabu kuwa ni viumbe wa kuogopesha kama huyu alioko mbele yangu.
“Toka..toka..toka" nilinong’ona kiwazimu, kana kwamba nafukuza ngedele shambani!. nikawa narudi nyuma hovyo, yule kiumbe alinitizama kwa macho yake mabaya yenye kufanana kabisa na mnyama aina ya kingkong niliye pata kumwona katika sinema, alinitizama kwa aina fulani ya mshangao! mimi pia nilishangaa mtazamo ule, labda aliona kitu kutoka kwangu ambacho hakutegemea.
Mkono wake ulio kuwa na nguvu aliunyoosha, na kwa maajabu mengine ule mkono ukawa unarefuka kama mpira kisha ukanikamata shingo kwa nguvu na kunivutia karibu yake.. "mamaaaaaa.maaaaaa nakufaaaa msaadaaa JINIIIIII!" nilipayuka hovyo, ila makelele yangu hayakufika umbali japo wa sentimita sitini,.
Nilikabwa kwa nguvu shingoni na yule kiumbe hadi nikawa sihemi.."ooh Yarabi niokoe mja wako mie" macho yalianza kuona giza dalili za kufa kwa kukabwa shingoni zikajidhihirisha, nikatepeta,. nguvu zikaniishia, yule kiumbe akaendelea kunikaba huku akishindilia kwenye shingo yangu vidole vyake vyenye makucha yaliyo komaa, hapo nikalegea nguvu zikanitoweka giza likafunika macho yangu.


Kwa mbali kabisa nikiwa sielewi A wala B fahamu zangu zikiwa zimepotea, lakini kama nukta kumi ama kumi na moja nikawa huru katika mikono ya yule kiumbe, nikawa nahema kwa tabu, nukta nyingine za kuhesabika nilihisi kama nashikwa mkono wangu wa kulia kwa kiganja kipana na kikubwa, halafu nanyanyuliwa kwa juu kwa nguvu nyingi, nilihisi naning'inia angani, huku mkono wangu wa kulia ukiwa umekamtwa kwa nguvu hadi mbavu zikawa zinauma..
Nilifumbua macho..
lahaula lakwata!. nilikuwa nimebebwa na kile kiumbe umbali wa mita takribani elfu tano angani.!
Hata macho yangu nilipotizama tena chini, niliona mji wa Kigoma kama kakijiji tu kadogo huku mataa ya umeme ya mji yakionekana kama mwanga wa vimuli muli ama vibatari vya wavuvi wanao onekana wakiwa maili nyingi nyakati za usiku katika bahali..
"Mungu uko wapi wewe Mungu wewe!. ona sasa hii nini sasa aaagh?" nililalama mno, nikajaribu kufurukuta lakini nikajikuta najisababishia maumivu mwenyewe kwani ule mkono wa yule kiumbe mwenye kupaa ulionekana kama sumaku, vile vile kuendelea kuleta usumbufu kwa kile kiumbe ni kujihatarishia maisha pengine hata kwa kuniachia ambapo nikianguka huko ardhini na kujibamiza, ni wazi, nitapasuka vipande vipande.
Kiumbe alizidi kwenda angani zaidi huku akienda kwa spidi kali mvumo wa upepo ukazidi kunitesa japo kule hapakuwa na mvua, kila lilokuwa linajili mbele yangu kwa kila wasaa ilikuwa ni kama zile hadithi za Swahili Simulizi na taa ya ajabu ama hadithi za e. Kulaya nimilzowahi kusimuliwa na babu yangu angali mdogo.
Na mpaka wakati huo, sikujua nini maana ya matukio yale. ****
Sijui ni muda gani ulitumika nikiwa naningi'inzwa angani mithili ya kifaranga cha kuku kilichobebwa na mwewe.
Ninacho kikumbuka nilijikuta nipo katika eneo fulani lenye joto kali na giza totoro bila shaka ilikuwa ni katika chumba kidogo, nasema ilikuwa ni katika chumba, kwa sababu hewa ya eneo hilo ilikuwa nzito na ndogo, katika papasa papasa yangu ya huku na kule kuna wakati niligusa kitu kama geti la chuma lililoKuwa limefungwa imara.
Wakati huo huo nilisika harufu ya nyama kama zilizo kuwa zikibanikwa, vilevile kwa mbali kulisikika sauti za kutisha na ngurumo nzito.
Lakini pia, wakati mwingine nilisikia sauti za watu wakiimba lakini nyimbo zilizo imbwa zilikuwa za hovyo hovyo zisizo na mvuto katika masikio ya mtu yeyote ambaye angepata bahati ya kusikia aina zile za za nyimbo..
Hii nini hii? kwanini haya yanatokea? ndio kusema nipo kwa mashetani sijui ujinini? kwanini niwe mimi?na kosa letu ni lipi hasa dhidi ya hawa mashetani? na wenzangu wengine wako huku? na kama wako huku wazima ama ndio washakufa kama Mpemba? na kama hawapo huku watakuwa wapi? yote ni maswali yaliniandama akilini mwangu, sikupata aina yoyote ya majibu.

Hadi wakati huo niliona ni kama ndoto tu mbaya ya kutisha inayo nipitia nikiwa katika usingizi wa pono, haiwezekani hadithi za mazimwi nilizo wahi kusimuliwa, eti leo iwe ndio maisha halisi ninayo kutana nayo!
Nikiwa bado katika tafakuri mara kishindo kikubwa kilisikika umbali fulani umbali ambao nilikuwa napata kusikia zile sauti za ajabu ajabu na nyimbo zisizo eleweka, na hata kile kishindo kilipo sikika mara ghafla ukimya ulitawala eneo zima kama kwamba palikuwa hakuna makelele ya aina yoyote eneo lile.
Mara nilisikia nyayo za kitu kikiwa kinakuja usawa ambao mimi nilikuwa nipo. Mtembeaji alifika hadi katika geti la chumba nilicho kuwa nimefungiwa kisha nikasikia chakara chakara za kufungua geti, kiumbe huyo sikuweza kumwona kabisa kutokana na giza lililokuwapo mule ndani.
Mara nilihisi kuguswa kwa kiganja cha yule kiumbe kisha nikashikwa kwa nguvu na kuvutiwa kwake.
Nilijikojolea.
Yule kiumbe alinikamata mkono pasina kuongea neno lolote kisha akawa ananiburuta kunipeleaka nisipo paelewa.
Nikiwa navutwa na yule kiumbe, yeye mbele, mimi nyuma, hatua kama kumi na mbili, tulifika eneo lenye mwanga wa mioto, ilikuwa ni vigingi vya mioto iliyo washwa kama mwenge na kuwekwa pembezoni mwa ukuta ambapo kulikuwa na sehemu malumu ya kushikia vile vingingi.
Kitu nilicho kigundu eneo lile, ni kwamba pale nilipo pelekwa palikuwa ni pangoni, kutokana na mzingira niliyo yaona ila sikujua ni mapango ya eneo lipi, kwani pamoja na kwamba kuwa ni mzawa wa Kigoma sijawahi kusikia eneo fulani kuna mapango, hivyo sikujua kabisa nipo katika mapango yaliopo eneo gani.
Yule kiumbe alikatisha kona kama mbili kisha tukatokea katika eneo pana kidogo ambapo kulikuwa na mazingira kama ya jiko huku upande wa kushoto mwa eneo lile kulikuwa na binadamu wa kawaida na majiko makubwa yalikuwa yamebandikwa masufuria makubwa huku kuni zilizo kuwa zikichochowe na wapishi hao binadamu zikiwaka kwa kasi.
Kulia mwa eneo lile kulikuwa na meza kubwa iliyo kuwa imetapakaa damu na nzi wakiwa wengi, na mbele yangu kulikuwa na chumba kidogo kilicho fungwa kwa kigeti kidogo chenye nondo ngumu, pia kilikuwa kimefungwa kwa kufuli imara.
Macho yangu yalirejea kwa wale binadamu wenzangu, sura zote zilikuwa ngeni, lakini moyo wangu ulipata ahueni kidogo kwani matumaini ya kukutana na binadamu wenzangu, tumaini lilijijenga moyoni mwangu kuwa uhai upo, japo sikujua kivipi watu hawa wawe huku tena wanaishi na viumbe wa ajabu kama huyu aliye nishika mkono tena bila wasiwasi wowote.
Wale watu hawakuonyesha kunijali hata kidogo. "heloooo!" nilitoa sauti kwa wale watu kuwaita, walicha kidogo kuchochoe kuni wakanitizama, "jamani huku wapi ninyi?" niliuliza, uso wangu nikufanya wenye huruma mbele ya macho ya wale binadamu waliokuwa wamevalia nguo nyeupe za kimapishi huku kichwani wakiwa na kofia nyeupe za duara, badala ya kunijibu wale watu miongoni mwao mmoja akamuuliza swali yule kiumbe, swali kwa rugha ya kiswahili, swali ambalo lilinikata maini, alisema, "vipi huyu nae binadamu jini kwani nyama yake siku hizi inaliwa?"
Ebwana weee! nilihisi wazimu unaniingia na kutoka! kama kuna siku mapigo yangu ya moyo yameenda kasi basi haishindi siku hii, kwani moyo ulinidunda kama mdundiko wa kizalamo!
Asalimia mia moja yule mpishi alihoji kuhusu mimi, japo katika baadhi ya maneno yake kuna neno ambalo sikujua nini maana yake ‘BINADAMU JINI’ yanii mimi ni mtu jini?.
Sikuelewa hapo.
Kwa mara ya kwanza nikasikia sauti ya yule kiumbe, asauti ilikuwa nzito haswaaa tena iliyo endana na mwonekano wake, jibu lake lilinifanya akili yangu ipoteze kabisa uimara kwa lugha ya kiswahili alimjibu hivi,
"Hapana, nyama yake hailiwi! huyu mchinjeni kisha mumbanike nyama yake itatumika kwa majaribio ya kutengeneza dawa ya ugonjwa wa Anofobia"
Nilianza kulia kama mtoto, nikawa nafurukuta kujinasua katika mikono ya kile kiumbe,lakini kiganja cha lile dubwasha kilinikamata imara kweli kweli. Alikuwa ni kama amekamata kifaranga cha kuku.
“Uwiiiiiii!..nakaufaaa mamaaa" nilipiga mayowe nikijinyonga na kulisuka suka lile jitu hata kwa kulivulumushia makonde, lakini ilikuwa ni kama namkuna tembo! Kwa jani la ufagio, haikutosha nikasogeza meno yangu katika mkono ule ulio nikamata kisha nikamuuma meno kwa nguvu.
Lakini wapi.
Ngozi ya lile jitu ilikuwa ngumu kama ya mamba!.
Nilivutwa kwa mvuto wa kawaida na yule kiumbe nilijibamiza katika vitu vilivyo kuwapo sakafuni kana kwamba nilivutwa kwa nguvu nyingi, kusema ukweli sijawahi kuona dude lenye miguvu kama lile!.
Nikakokotwa hadi katika chumba kilicho kuwa mbele yangu, kisha yule kiumbe akafungua akiniachia mkono, akawa anafungua kufuli la pale getini.
Nikakurupuka na kutoka ‘mkuku’ huku nikipamia vitu vilivyo kuwa 'shabarabaghala', ajabu ni kuwa hakuna mtu aliye hangaika na mimi, yanii naweza nikasema wale watu walikwisha zoea kuona purukushani za watu eneo lile, hakuna aliye jali mbio zangu, kila mtu aliendelea na shughuli yake, hata yule kiumbe pia, aliendelea na kufungua lile kufuli pale getini.
PLAY STORE - SWAHILI SIMULIZI APP
Nilichoropoka mule ndani, nikapita katika kona mbili tatu, kisha nikatokea katika kijinjia chembamba ambacho kilikuwa na mioto inayo waka kama mwenge, nikazidi kukimbia kwa kasi kuelekea mbele, kasi niliyo kuwa nayo bado niliona haitoshi kwani suruali yangu nayo ilikuwa inanisumbua ilikuwa inavuka.
Kama ingetokea bahati ya kuniona, ungeshuhudia namna nilivyo kuwa nikitweta hovyo, mkono wangu nikiwa nimekamatilia suruali yangu iliyo kuwa inanivuka, huku kila sekunde nikigeuza macho yangu nyuma kuona niko umbali gani dhidi ya adui aliye taka kunichinja na nyama yangu kuibanika!. eti nyama yangu itafanyiwa majaribio ya ugojwa wa anofobia, ugonjwa ambao sijawahi kuusikia hapa duniani.
Nilizidi kujisukuma kwa mbele, huku nikihema kwa pupa hofu ikiwa kwa kiwango cha mwisho kabisa.
Nikiwa umbali fulani mara nikawa nasikia zile sauti za ajabu ajabu na nyimbo zisizo eleweka, kile kinjia kilikuwa kirefu hata nisiweze kuona mwisho wake, na mita kama kumi niliona kuna kona upande wa kulia, nikaongeza kasi nifike katika kona ile ili niachane na ile njia iliyo nyooka, kwani kuendelea kukimbia nikiwa katika njia ya namna ile isiyo onekana mwisho ni hatari.
Vilevile kama mtu angesimama mwanzo wa ile njia basi lazma angeweza kuniona kwa mbali nikiwa nakimbia kiwazimu.
Nikaongeza kasi ya mbio kuifikia ile kona.
Ile nafika tu...!
Ghafla….. nini tena.. ni simulizi yenye mambo ya kutisha, vita, utam… n.k fika whatsapp +255 758 018 597

Post a Comment

1 Comments

Karibu sana, tuma ujumbe whatsapp +255 758 018 597 kujipatia simulizi zetu

Emoji
(y)
:)
:(
hihi
:-)
:D
=D
:-d
;(
;-(
@-)
:P
:o
:>)
(o)
:p
(p)
:-s
(m)
8-)
:-t
:-b
b-(
:-#
=p~
x-)
(k)