Nilikuwa nimeongozana na mke wangu tukitokea dukani eneo lile
la ugenini nikiwa busy kwenye simu yangu huku nikiongea na mke wangu ambaye
alikuwa nyuma yangu akinisemesha hili na lile. Mara nikagundua hali isiyo ya
kawaida, mke wangu alikuwa kimya ghafla.. nikageuka haraka kutaka kujua nini
kilimfanya awe kimya namna ile lakini cha ajabu sikumuona mke wangu.
"khaaa, kabaki wapi huyu mwanamke?" nilijikuta nikiuliza kwa sauti
ilhali nilijua fika kuwa nilikuwa peke yangu eneo lile lenye kiza cha kutosha.
Uamuzi nilioufikia haraka ni kuamua kurudi nyuma kujaribu kumtafuta huku
nikimpigia simu kwa maana nakumbuka alitoka nyumbani na simu yake. kitu cha
ajabu simu yake iliita nyuma yangu baada ya kuwa nimetembea hatua chache tu,
niligeuka nikaufuata muito ule wa simu ambao nilikuwa nikiujua kuwa ni wa simu
ya mke wangu... kweli ilikuwa simu ya mke wangu ikiwa pale chini ikiendelea
kuita, nilishikwa na bumbuwazi kwa sekunde chache nisijue hata cha kufanya
kisha nikaiokota ile simu na kuanza upya safari ya kurudi eneo lile la madukani
kujaribu kuona kama naweza kumuona mke wangu.
Nilitembea huku nikiangaza huku na huko nikiamini pengine
ningemuona mke wangu lakini mpaka nafika eneo lile la maduka sikuwa nimemuona.
Nikajaribu kuvuka eneo lile na kuangalia maeneo ya mbele
zaidi ila sikumuona.
Akili ikaniambia labda atakuwa amekwenda nyumbani, nikakimbia
mpaka nyumbani ila mlango ulikuwa umefungwa kama ambavyo tuliuacha, mke wangu
hakuwepo na funguo alikuwan azo yeye. Sikuwa na sehemu nyingine ya kumuangalia
kwa maana tulikuwa hata hatujazoeana na majirani.
Moja kwa moja nikaenda mpaka duka lile ambalo tulikuwa
tumenunua bidhaa dakika chache zilizopita kwani ndilo duka pekee ambalo
tulikuwa tukinunua kwa muda wote wa siku tatu tangu tuhamie mji ule. Hata
muuzaji wa duka lile tulikuwa tumeanza kuzoeana hivyo sikuwa na mtu mwingine wa
kumfuata wakati ule zaidi yake.
“samahani Mangi” nilianza kumsemesha mara baada ya mteja
aliyekuwa akamuhudumia kuondoka... “aisee mke wangu hajafiaka hapa?” niliuliza
nikilingojea jibu kwa hamu huku nikitamani awe na chochote cha kusema ambacho
kingesaidia kumpata mke wangu kwa maana hofu kubwa ilikuwa imeniingia tayari..
Mangi alionekana kunishangaa kidogo kisha akauliza..
“wewe si umeondoka hapa na mke wako hata dakika kumi
hazijaisha?” kufika hapo nikachoka kabisa na kujikuta nikikaa kwenye benchi
ambalo lilikuwa nnje pale dukani. Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka kiasi ambacho
kilimshangaza Mangi ambaye wakati huo alikuwa akijaribu kunisemesha lakini hata
sikumbuki alikuwa anaongea nini kwa maana akili yangu hata haikuwa pale na wala
sijui ilikuwa wapi.
Kugutuka nilimuona Mangi akiwa amesimama mbele yangu pamoja
na watu wengine ambao walionekena kuwa wenyeji wa eneo lile wakitaka kujua nini
kilikuwa kimetokea.
“Kijana hebu tueleze hali ambayo imetokea pengine tunaweza
kusaidiana mawazo na jambo likawa jepesi” aliongea mzee mmoja wa makamo ambaye
sikumfahamu ila moja kwa moja nikajua Mangi alimuita ili kuja kusaidia baada ya
kuniona katika hali ile isiyoeleweka.
Nilijikaza nikawasimulia mkasa uliotokea, wakati naendelea
kuongea watu walikuwa wanazidi kuongezeka.. mpaka namaliza kuongea kulikuwa na
kundi kubwa sana, wake kwa waume.
“Jamaniiiii hali hii mpaka lini?” ilikuwa sauti ya mama mmoja
mtu mzima ambaye alikuwepo akisikiliza maelezo yangu, kauli ile iliniacha njia
panda.. inamaana matukio ya namna hii ni ya kawaida kutokea eneo lile? Nilikuwa
nikijiuliza. Watu
ambao walikuwepo pale pia hawakuonekana kujiuliza ni wapi
alipotelea mke wangu badala yake walionekana kunionea huruma.
Pemebeni nilimuona mzee yule ambaye alinitaka kuwaelezea
ambacho kilinisibu akishauriana na wanaume wengine watatu kisha wakaja pale
nilipo..
“Tumpelekeni kwa mzee Miale” aliongea yule mzee, wakanisaidia
kunyanyuka na safari ya kuelekea kwa mzee Miale ambaye sikujua ni nani wala
tunaenda kufanya nini kwake ikaanza.
Kwakweli nilikuwa nimechanganyikiwa nikajikuta nafuata kila
ambacho naambiwa bila hata kuhoji.
Tulifika kwa mzee Miale tukabisha hodi na kupokelewa na mama
mtu mzima kidogo.
“Karibuni jamani, kwema?” alitukaribisha mama yule akiwa na
mshtuko nadhani ilitokana na wingi wa watu ambao tulikuwa tumeongozana nao.
“Sio kwema sana shemeji, huyu bwana tumemkuta?” aliongea mzee
mmoja kwa niaba ya kundi lile.
“Hapana, huyu bwana ameenda kwenye
shughuli zake huko Michese ila atarudi asubuhi” alijibu yule
mama ambaye nilikuwa nimegundua kuwa alikuwa mke wa mzee Miale. Yule mzee
ambaye tulikuja naye akamchukua yule mama wakakaa kando kidogo na kuongea,
nadhani alikuwa akimuhadithia kilichonikuta. Baada ya muda mfupi wakasogea
ambapo tulikuwa tumesimama na yule mama akaongea..
“Pole kwa yaliyokukuta mwanagu, jikaze ndio ukubwa huo”
akanitazama, nikaitikia kisha akaendelea..
“Sasa wewe nenda kapumzike kesho mida ya
saa mbili uje mzee atakuwepo” aliongea yule mama nami
nikaitikia.
Tukaondoka njiani tukigawanyika kila mmoja akishika njia ya
kuelekea kwake mpaka nikabaki na vijana wawili ambao tuliendelea kuongozana..
“Pole sana kaka, mimi ni jirani yako bwana, nakaa ile nyumba
yenye rangi ya kijani kulia mwa pale kwako” aliongea mmoja wa wale vijana
wenzangu huku mwingine akituaga na kufuata njia ambayo ilimuhusu.
“Asante aisee” nilimjibu tukaendelea na safari huku
nikijaribu kudodosa juu ya ambacho anadhani kitakuwa kimempata mke wangu.
“Mimi ni mbumbumbu juu ya hili kama ulivyo wewe, ukifika kwa
yule mzee kesho nadhani unaweza kupata majibu mazuri” alinijibu wakati huu
tukiwa tumefika kwangu tukaachana.
Nilitembea hatua chache kuelekea ulipo mlango wa kuingilia
nikakumbuka kuwa mlango ulikuwa umefungwa na funguo alikuwa nazo mke wangu,
nikafikiri kwa muda na kisha kuamua kuwa kama simu iliachwa pale basi pengine
na funguo ipo maeneo yale ila sikuiona kwakuwa kulikuwa na giza, hivyo nikaamua
kurudi eneo lile nikaitafute kwa kutumia tochi ya simu ya mke wangu ambayo
ilikuwa na mwanga mzuri tu.
Saa kwenye simu ilikuwa inaonesha kuwa ni majira ya saa sita
kasorobo usiku, nikatembea polepole kuelekea eneo ambalo alipotelea mke wangu,
nikafika na kuwasha tochi ya simu kisha nikaanza kuangaza kuitafuta funguo ya
mlango wa nyumbni kwangu lakini nilishtushwa sana na ambacho nilikiona kama
hatua tatu mbele ya ambapo nilikuwa nimesimama, zilikuwa ni nguo za mke
wangu......
Nilisogea mpaka zilipokua zile nguo nikazikagua na kugundua
kweli zilikuwa nguo za mke wangu, tena zote mpaka za ndani, niliogopa sana na
kuanza kuhofia ambacho kilikuwa kimempata mke wangu kipenzi.
Wakati naendelea kumulika nikaiona na funguo ambayo ndio
chanzo hasa cha mimi kwenda eneo lile wakati ule, nikaiokota pamoja na nguo za
mke wangu na kuanza safari ya kuelekea nyumbani.
Nilifika nyumbani nikafungua mlango na kuingia ndani kisha
nikajilaza chali kitandani, nilikuwa nimechoka sana kuanzia mwili mpaka akili,
nikachukua simu yangu na kupiga namba za baba yangu, niliamini ni mtu pekee
ambaye angeweza kunifaa kwa wakati ule kama ambavyo amenifaa mara zote
ninapohitaji msaada wake wa kimawazo...
Simu ile iliita kwa muda lakini haikupokelewa, nikaangalia
saa na kugundua ilikuwa saa sita na robo usiku, bila shaka atakuwa usingizini
na mara zote huiweka simu yake silent anapolala.
Niliachana na kupiga simu nikajaribu kulala lakini haukuwa
usingizi wa maana, akili yote ilibaki macho ikijaribu kuvuta upya taswira ya
tukio zima ambalo lilikuwa limetokea...
Nilijikuta nikiamini tukio lile lilikuwa likihusika na
masuala ya kishirikina, mambo ambayo sikuwa na uzoefu nayo hata kidogo,
niliishia kuyasikia tu kwa watu.
Hali ikawa hivyo usiku kucha, kila saa nikijaribu kuangalia
saa yangu nikitamani kukuche nianze hatua za kumtafuta mke wangu...
Sasa saa ilionesha kuwa ilikuwa saa 11 na dakika 5 alfajiri,
simu yangu ikiwa inaita, nilikurupuka haraka nikaichukua na kumuangalia
mpigaji, alikuwa ni baba yangu, ambaye nadhani ndio alikuwa anaamka na kukuta
“missed call” yangu ile ya usiku mnene. Nilipokea haraka haraka na kuanza
kuongea na baba ambaye moja kwa moja alijua kuna tatizo kutokana na kumpigia
muda ule ambao si muda wa kupeana salamu za kawaida.
Nilimuelezea baba kila kilichokuwa kimetokea naye
akashangazwa sana na hali ile, alikaa kimya kwa muda, nadhani alikosa chochote
cha kusema kisha akaongea “Jikaze mwanangu, kukicha nenda kwa huyo mzee ukaone
kama atakuwa na msaada wowote, mimi nitaondoka na basi la kwanza hapa nadhani
majira ya saa saba mchana tutakuwa pamoja” tukaagana, akakata simu nami
nikajiinua kutoka pale kitandani ambapo sikuweza kupata usingizi usiku kucha.
Nikaingia bafuni, nikajimwagia maji ili kuchangamsha mwili
tayari kwa kwenda kwa mzee Miale, wakati nikiwa nakoga nikajiuliza kwanini
sikuwa nimeripoti tukio lile katika kituo cha polisi, nikajiona nilikuwa mzembe
hivyo nikaoga haraka haraka kisha nikatoka na kuvaa, safari ya kuelekea kituo
cha polisi ikaanza kwa kutumia pikipiki yangu, wakati huo ilikuwa ni majira ya
saa 12 za asubuhi nikaamini nitawahi kurudi na kwenda kwa Mzee miale kwa
wakati.
Nilifika kituoni nikajitambulisha na kuelezea kilichotokea,
askari walichukua maelezo yangu wakayaandika na kuniruhusu kuondoka,
nilishangazwa kuona hawakulichukulia jambo lile kama jambo kubwa sana, sasa
niliamini tukio langu halikuwa la kwanza katika jamii ile. Nikaondoka na
kuelekea kwa mzee Miale.
Nilifika nikapokelewa na mzee ambaye umri wake ulionekana
kuwa si chini ya miaka 70, ambaye nilimkuta amekaa peke yeke kwenye kiti cha
kizee pale nje, “Shikamoo mzee, sijui wewe ndo mzee Miale?” nilisalimia
akaitikia nikamuuliza na swali ambalo alilijibu kwa kukubali kuwa ndio yeye,
nami nikajitambulisha na akanitambua haraka kwa maana alikua tayari
ameshaelezwa juu yangu, alinichukua tukaingia ndani kisha akaanza kunieleza juu
ya ambacho kimemtokea mke wangu, akianzia kunipa historia ya miaka mingi sana
iliyopita...
“Zamani eneo hili lilikuwa ni himaya ya wachawi wenye nguvu
kubwa sana, wachawi kutoka maeneo mbalimbali walikuja katika eneo hili na
kujifunza taaluma hiyo kisha wakatoka wakiwa na uwezo mkubwa sana.
Wachawi hao walikwenda kwenye maeneo yao na kuwa wasumbufu
katika jamii, na kama nilivyokueleza walikuwa na nguvu sana hivyo mbinu za
kupambana nao hazikuwa zikifanikiwa. Ulifikia wakati watawala wa maeneo
mbalimbali walikutana na kujaribu kushauriana nini kifanyike juu ya wachawi
ambao walikuwa kero kubwa kwa wananchi wa himaya zao, tawala zile zikakubaliana
kuwa eneo hili ambalo ndilo lilikuwa makao makuu ya shughuli hizo haramu
liteketezwe lote, mipango ikapangwa wakishirikiana na waganga wa kienyeji ambao
walikuwa na mbinu za ziada na ikabainika siku ambayo wachawi wote hukutana
katika eneo lile, wakaamua kuitumia siku hiyo kwenda kuwateketeza wote, lakini
kwa bahati mbaya habari zikavuja na kuwafikia wachawi wale ambao waliutumia
uchawi wao kujikinga, wakajenga himaya yao ndani ya eneo hili kisha wakafanya
zindiko kubwa kuhakikisha himaya yao hiyo haitokuwa ikionekana na mtu yeyote,
hivyo watu wale waliokwenda kwa ajili ya kuwateketeza walikuta mji huu hauna
mtu hata mmoja, ikabidi wataalamu ambao walikua nao wapige ramli na kugundua
nini kilikua kimetokea, wakagundua zindiko hilo la wachawi hivyo nao wakafanya
ufundi wao kuzuia himaya hiyo ya siri ibaki hukohuko na isiingiliane na himaya
hii, kisha wakafanya utaalamu mwingine ili watu wa himaya hiyo ya siri
wasizaliane wakiamini watakuwa wakifa bila kuzaliana hatimaye himaya hiyo
itatoweka..
Maisha yakaenda hivyo kwa muda kidogo lakini baadae watu wa
himaya ile ya kichawi wakapata namna ya kuwa wanapenya na kuja himaya hii mara
chache.
Baadae wakaamua kuwa ikitokea mtu amekufa himayani mwao basi
hutoka nje ya himaya yao na kumchukua mtu mwingine ili aende kuziba nafasi ile,
lakini ilikuwa ngumu sana kwa mtu ambaye ametokea huku nje kuishi kama ambavyo
wao walitaka hivyo wakaja kugundua njia nyepesi na kumfanya mtu awe wa kule
(mtu wao) na kisha aishi kama wao ni mtu huyo kuzaliwa katika ardhi yao, kwa
kua hawakuweza kuzaliana kutokana na laana ile ya wazee wa zamani wakaamua kua
wawe wanakuja huku na kukamata wanawake wajawazito kisha wanawapeleka katika
ardhi yao ili mtoto akazaliwe katika ardhi yao na kisha hua wa kwao kabisa..”
alitulia kidogo akaniuliza.
“Ni kweli mkeo alikuwa mjamzito??”, nami nikamjibu kua ni
kweli, mke wangu alikuwa na ujauzito wa miezi miwili.
Sasa nilikuwa nimejua nini kilikuwa kimempata mke wangu.
“Nawezaje kumpata mke wangu mzee?” nilimuuliza mzee Miale
huku moyoni nikiwa nasali kuwe na njia ya kufanikisha hilo......
Mzee Miale aliniangalia kwa upole kisha akasema “watu kutoka
dunia yetu hii huwa hawaingii mji ule wa siri ingawa wa kutoka kule huja huku,
unadhani mkeo atarudije ukizingatia habari ambayo nimekueleza?”
Kauli za mzee Yule zilizidi kunichanganya nikajiona kama
nilipoteza muda kuja pale. Nilijikuta machozi yakinitiririka bila kizuizi
chochote mzee yule akinishuhudia bila hata ya kuwa na msaada wa kunipa.. “huu
ni uonevu, bora wangechukua kingine chochote lakini sio mke wangu” niliongea
kwa hasira, mzee miale akanitazama kwa masikitiko kisha akaongea “jikaze tu
mwanangu, utafanya nini sasa?” nilianza kuichoka ile kauli ya nijikaze ambayo
nilikuwa nimeisikia mara nyingi sana toka kumpoteza mke wangu kipenzi siku
chache tu baada ya ndoa yetu, niliona kama watu wale waliokuwa wakinitaka
nijikaze walikuwa hawaelewi ni kiasi gani nilikuwa nikiumia.
“nitahakikisha nampata mke wangu kwa gharama yoyote, sikubali
hata kidogo nasema, nitapambana mpaka kieleweke” nilisema huku nikisimama ,
machozi yalikuwa yamenifika shingoni. Mzee Miale alinisihi kuwa mtulivu lakini
sikuwa nikitaka tena hata kumsikiliza kwa maana niliona msaada wake ulikuwa
umeishia pale kwenye kunijuza mahali ambapo mke wangu angeweza kuwepo wakati
ule. Nilimuaga nikaondoka na kuelekea kazini kwangu ambapo nilitegemea kukutana
na rafiki yangu bwana Anthon Matovu ambaye nilitegemea tunaweza kushauriana na
kujua pa kuanzia, kwa kutumia pikipiki yangu haikunichukua muda sana nikawa
nimefika kazini na kukutana na bwana Matovu nikamuomba tutoke kidogo ofisini kwa
ajili ya mazungumzo mazito kidogo, naye akatii tukatoka na kwenda kukaa kwenye
glosary ambayo ilikuwepo pale karibu tukakaa na nikamuelezea tatizo kubwa
ambalo lilikuwa likinikabili.
Habari ile ilimshangaza na yeye ila akashauri twenda kwa
mtaalamu wa masuala haya ya kienyeji ambaye alikuwa akimfahamu. Nilijaribu
kumueleza kuwa jambo hili pengine lisingeweza kutatuliwa na mtaalamu huyo ila
akasisitiza kuwa mzee huyo anayepatikana kijiji cha Ihihi ni mjuzi hasa na
lazima atalimudu jambo lile. Tukakubaliana kwenda Kijiji hicho kesho yake
asubuhi.
Tukarudi ofisini, nikafanya utaratibu wa kuomba likizo ya
dharura, nikaomba likizo ya miezi mitatu bila malipo nikijieleza kuwa na
matatizo ya kifamilia ambayo yanahitaji muda wa kutosha kuyatatua na
nikafanikiwa.
Nilirudi nyumbani nikajipikia chakula na kukaa kujaribu kula
lakini sikuweza, niliyaona maisha yangu kuwa magumu bila mke wangu pale
nyumbani, nilitamani tu kesho ifike nipelekwe huko kwa huyo mganga nikaone kama
anaweza kunisaidia kumpata mke wangu.
Wakati huo nilipata ujumbe mfupi wa simu toka kwa baba ambaye
alikuwa akinijulisha kuwa alikuwa amekaribia kufika stendi ya mabasi nami
ikanibidi kwenda kumpokea. Nilimpokea baba tukaenda nyumbani ambapo tulikaa
nikamuelezea ambapo nilikuwa nimefikia katika harakati za kumtafuta mke wangu,
tukakubaliana kuwa kesho yake tungeenda pamoja kwa mganga huko Ihihi.
Tuliongea mengi, sana sana alikua akinifariji na kunitaka
nijikaze kiume akiamini kuwa hili litaisha salama na mke wangu atarudi kuishi
nami.
Kutokana na uchovu baba alitangulia kuchoka akaniaga na
kwenda kulala akiniacha mimi nikiangalia TV ingawa kwa kweli hata sikuwa
nikiona nini kilikuwa kikiendelea kwa maana akili yangu hata haikuwa pale.
Majira ya saa 7 usiku nilihisi kuchoka nikaamua kwenda chumbani kujipumzisha,
nilifika nikajitupa kitandani kama nilivyokuwa na kupitiwa na usingizi.
Nilishtuka kutoka usingizini kutokana na upepo mkali ambao
ulikuwa ukivuma mule chumbani, upepo ule ulifikia kusukuma vitu vyepesi
vikaanguka na vingine kugongana mpaka kukawa kuna hali ya kelele mule chumbani,
niliamka haraka nikakaa kitandani na kusikilizia hali iliyokuwa ikiendelea,
mara chumba kilijazwa na mwanga mkali sana ingawa taa haikuwa ikiwaka, mwanga
ule ulitosheleza kuona kila kitu mule ndani kama vile ilikuwa mchana.
Kwenye pembe mojawapo ya chumba kile nilimuona mtu akiwa
amechuchumaa nikashituka sana, ilibaki kidogo nikimbie lakini mtu yule aliamka
pale haraka sana akasimama akiuziba mlango, ili nisitoke maana kupita ilikuwa
ni lazima nimtoe yeye pale mlangoni.. “kama unataka kumpata mkeo tulia na
unisikilize kwa makini” aliongea mtu yule ambaye alikuwa ni mzee kiasi. Ingawa
nilikuwa bado naogopa nilijikaza na kukaa kitandani kwa upole. “mimi ndo mtu
pekee ambaye naweza kukusaidia kufika alipo mkeo kwenye dunia hii” aliongea mtu
yule akinisogolea kwa tahadhari kubwa. “tafadhali nisaidie kumpata mke wangu,
niko tayari kufanya chochote ili kuonana tena na mke wangu” nilisema katika
hali ile ya uoga na mtu yule akawa amefika kabisa mbele yangu na sasa niliweza
kuiona hata sura yake ambayo ilikuwa ya mtu wa kawaida tu, wala haikuwa
ikitisha. “kumpata mkeo inakupasa kuwa jasiri sana, ni lazima uingie MUIFUFU”
alielezea mzee yule. “MUIFUFU ndo wapi mzee wangu?” niliuliza kwa shauku ya
kutaka kujua nini napaswa kufanya ili kumpata mke wangu, nilikuwa tayari kwa
lolote. “Muifufu ni mji wa siri ambao upo ndani ya mji huu, huko ndiko mkeo
aliko” alisema mzee nami nikaelewa kuwa alikuwa akiuzungumzia mji ambao
nilielezewa kuuhusu na Mzee Miale. “niko tayari mzee wangu, nawezaje kufika
huko” niliongea nikionesha nia thabiti ya kwenda sehemu hiyo kwa kua ndiko
aliko mke wangu na mwanangu ambaye yuko tumboni ambaye sikutaka kabisa aishi
maisha ya huko kwa mashetani. Mzee yule aliniangalia akatabasamu, kisha
akaongea “kwenda Muifufu sio jambo la mchezo, wengi ya wanaoishi huko ni
wachawi na ili kufanikiwa ndani ya mji ule ni lazima na wewe uwe mchawi”
aliongea mzee yule ambaye bila shaka na yeye alikuwa mchawi. Nilishituka sana
nikawaza kuhusu mimi kuwa mchawi na nikaingiwa na uoga lakini baada ya
kukumbuka kua ndio njia pekee ya kumrudisha mke wangu kwenye maisha yetu ya
pamoja nilijikuta nikijibu.. “niko tayari mzee wangu, niko tayari kwa chochote”
Yule mzee aliniangalia kwa utulivu kisha akasema
"nakuachia siku nzima ya kesho kufikiria kama kweli uko tayari kwa
hili" kisha akaanza kurudi kinyumenyume na giza likarudi kama ilivyokuwa
awali
"NGOJAAAAAAA USIONDOKEEEEEE" Nilisema kwa sauti
baada ya kugundua kuwa mzee yule alikuwa anaondoka.. "ongea haraka,
napaswa kuondoka hapa
kabla anga halijafunga" aliongea nami nikaendelea ingawa
sikuelewa alikuwa na maana gani kuhusu anga kufungwa "niko tayari mzee,
tunavyozidi kuchelewa napata mashaka juu ya hali ya mke wangu huko
aliko" nilisema kwa hali ya kubembeleza, kwakweli
sikuhitaji muda zaidi wa kufikiria nilikuwa tayari kufanya chochote. "mkeo
ni
mjamzito, tena mimba yenyewe ndo kwanza ina miezi miwili,
wanawake
wajawazito huwa wanaishi kama malkia huko Muifufu, huwa
hawapati shida
yoyote ingawa wana maisha kama ya kinyonga" aliongea na
mwishowe
akaishia kunichanganya tena, "maisha kama ya kinyonga?
una maana
gani?" nilijikuta nikipata swali lingine na kumuuliza
tena... "hilo nitakuelezea wakati mwingine, kuna miezi saba kabla mkeo
hajajifungua na ndani ya wakati wote huo atakuwa na maisha ya amani sana, ila
wazo la kwenda kwa mganga kesho uliondoe kabisa kwa maana uchawi wa huku si
kitu kulinganisha na uchawi wao, ukienda kwa mganga akafanya chochote
watagundua kama unawafuatilia na hapo wataanza kukufuatilia
kila hatua
na mipango yetu yote itajilikana kisha hakuna ambacho utaweza
kufanya... KWAHERI" Alimaliza kuongea akamalizia na kuaga bila
kunisikiliza.. "HAPANAAAA, SUBIRIIIII" nilisema haraka nikitaka
kumuuliza zaidi angalau hata nijue nawezaje kumpata iwapo
nitamuhitaji
tena lakini upepo kama ambao ulivuma wakati anakuja ukavuma
tena na kisha kukawa kimya sana, nikaamka kwa kasi na kwenda kuwasha taa kisha
nikaangaza huku na huko ndani ya chumba lakini nilikuwa pekeyangu ndani ya
chumba kilichovurugiza kama vile wamepita ng'ombe maeneo yale.
Sikuwa na chakufanya zaidi ya kutoka chumbani nikaenda
kumuamsha baba
na kumuelezea juu ya ambacho kimetokea, baba aliniambia kuwa
alisikia nikiwa naongea na mtu akadhani nilikuwa naongea na simu kwa maana
ilikuwa ikisikika sauti yangu bila ya ambaye naongea naye.
Tulishauriana na baba kuhusu kwenda ama kutokwenda kwa mganga
kesho
yake, mimi nilikuwa nikishauri tusiende lakini baba alikuwa
anasisitiza twende kwakuwa yeye hakumuamini mzee yule ambaye aliingia chumbani
kwangu "vipi kama mzee huyo ni kundi lilelie la wachwawi waliomchukua mkeo
na sasa anakutisha ili tusiende kwa mganga huyo
kwakuwa wanajua nguvu zake?" baba aliuliza swali ambalo
kwakweli lilikuwa swali la msingi, kwa kiasi fulani nikaona yuko sahihi. Lakini
nilikuwa naogopa pia kwenda kwa mganga yule kwamaana kama maneno aliyoyasema
mzee yule ni yakweli basi nitakuwa napoteza nafasi ya kumpata mke wangu. Mwisho
tulikubaliana kuwa asubuhi tukamuone mzee Miale labda anaweza akawa anajua kitu
chochote juu ya mzee yule aliyenitokea chumbani.
nikaachana na baba na kurudi chumbani ambapo sikuweza kupata
usingizi, nikachukua laptop yangu na kuanza kuperuzi kwenye internet.
Wakati nikiendelea kuperuzi nikiwa sina kitu maalumu ambacho
nimekilenga nikakumbuka kauli ya mzee yule kuwa maisha ya mke wangu ni kama ya
kinyonga, nikajiuliza mdudu yule mbaya wa sura ana kipi kinachofanana na maisha
ya mke wangu, kitu pekee ambacho najua ni maarufu kuhusu kinyonga ni kuwa ana
uwezo wa kuiga rangi yoyote aitakayo je mke wangu amefikia huko? nikajikuta
nikiingia google na kusearch juu ya maisha ya kinyonga. Baada ya dakika 5 tu
nilijikuta nimekipata ambacho nilikuwa nakitafuta, sehemu hii ni sehemu ambayo
ilikuwa ikielezea kuwa kinyonga huwa akizaa anakufa na mtoto
anaishi..
Nikakumbuka maneno ya mzee yule kuwa kabla ya kuzaa mke wangu
ataishi kama malikia kwakuwa ana mimba, nikaelewa kuwa ukinyonga utampata pale
atakapozaa kwa maana atakufa yeye na kubaki mtoto, uoga ukaongezeka maradufu,
nikatamani wakati huo ningekuwepo alipo mke wangu niweze
kumuokoa kwenye dhahama ile lakini halikuwa jambo lililo
ndani ya uwezo wangu, nikaishia kujifariji kuwa bado kuna miezi saba mpaka
kufikia wakati huo.
Ilikuwa majira ya saa mbili asubuhi nikiwa nimekaa na baba
kwenye kasebule kale kadogo cha mzee Miale tukimsubiri aje baada ya kupokelewa
na mjukuu wake na kuambiwa kuwa babu alikuwa akioga!,
tulisubiri kwa dakika kama kumi kisha mzee Miale alijumuika
nasi na mazungumzo yakaanza kwa kumtambulisha baba yangu kisha nikamuelezea juu
ya ujio wa mzee yule wa usiku pamoja na maonyo yake.
Taarifa ile ilionekana kumshitua mzee Miale ambaye aliniuliza
maswali mbalimbali nami nikayajibu kisha akaonekana kugundua kitu..
"Huyo aliyekuja kwako ni Mnaro,mtoto wa mzee Magugi
ambaye ni matwala wa
Muifufu" baba alinitazama kisha akanambia "si
nilikwambia? wote hawa
ni kitu kimoja" lakini mzee Miale akamkatisha "hawa
sio kitu kimoja
hata kidogo, Mnaro amemuasi baba yake kitambo sana na
kukimbia Muifufu" alisema mzee Miale kisha akaendelea, "Inasemekana
Mnaro na baba yake bwana Magugi wana ugomvi wa masuala ya kimapenzi, Magugi
alipora binti ambaye Mnaro alikuwa akimpenda toka utotoni na kumfanya mke wake
wa 28, Mnaro alimuomba sana baba yake kumuachia mke huyo tu na ahangaike na
wengine wote waliobaki kama angewahitaji ila baba yake alikataa akidai kuwa
iwapo Mnaro angeishi na mwanamke yule angekuwa
mdhaifu sana juu ya mwanamke huyo na hata kutawaliwa na
hatimaye kutoa siri ambazo watu wa Muifufu hawazijui isipokuwa Magugi na
mwanaye
Mnaro ambaye alikuwa akimuandaa kuja kuwa kiongozi wa Muifufu
baadae.
Kutokana na hasira za kunyang'anywa ambacho alikuwa akiona ni
haki yake Mnaro alifanya jaribio la kumuua baba yake ambalo lilishindikana
kisha akakimbia Muifufu, askari wa mzee Magugi kutoka Muifufu walikuja mara
kadhaa kwenye ardhi hii kumtafuta Mnaro lakini hawakufanikiwa, pengine ni
kutokana na mbinu nyingi ambazo alikuwa
nazo kwa kuwa baba yake alimfundisha mengi akimuandaa kuja
kumrithisha
uongozi, hivyo Mnaro hakuwahi kuonekana toka wakati huo
lakini naamini ni yeye ambaye alikuja kwako usiku kwa maana hakuna mtu mwingine
ambaye anajua habari za Muifufu zaidi yake" mzee Miale alimaliza maelezo
yale na mara ikasikika sauti ambayo haikujulikana ilikotokea
ikisema "na kama baba yangu angejua kuwa kuna mtu
anaijua historia yake
namna hii basi usingekuwa hai mzee Miale"
sote tukakaa kimya na kuisikiliza sauti ile ambayo
iliendelea,
“Nimekuwemo ndani ya ardhi hii nikiishi maisha ya upweke kwa
muda mrefu lakini nikiwa na ndoto kubwa ya kuja kutawala Muifufu. Tumaini pekee
la kufanikisha mpango wangu ni kumtorosha mpenzi wangu ambaye kwa sasa anaishi
kama mke wa baba yangu. Kabla ya kwenda kufanya jaribio la kumuua baba yangu
niliongea na na mwanamke yule nikamwambia ambacho nataka kufanya kwaajili ya
mapenzi yetu na ambacho nitafanya iwapo nisipofanikiwa, tukakubaliana kuwa
endapo nisipofanikiwa yeye ataolewa na baba yangu na kuigiza kama mke mwema
mpaka hapo mimi
nitakapofanikiwa kwenda kumchukua huku wakati wote akiyasoma
mazingira ya baba yangu na kupata njia ambayo itatuwezesha kuuangusha utawala
wake wa kikatili ndani ya Muifufu, baba yangu anaamini mwanamke yule amefutwa
kumbukumbu zote kwenye kichwa chake kama ambavyo hufanywa wakazi wote wa
Muifufu lakini akili ya mwanamke huyo iko sawa na anakumbuka kila kitu kwa
maana niliikinga vilivyo kabla ya kukimbia Muifufu” sauti ile ilinyamaza kwa
muda wa sekunde kumi na tano nami nikauliza huku nikiwa sijui kama mtu yule
bado yupo ama ameondoka
tayari “kwahiyo watu wote wa huko Muifufu hufutwa kumbukumbu
kwenye
akili zao?” sauti ile ikajibu.. “ndio, hata ukikutana na mke
wako leo hawezi kukumbuka wewe ni nani, hakuna kitu hata kimoja ambacho
anakumbuka zaidi ya kuamini kuwa Magugi ndio kila kitu katika maisha yake na
anapaswa kuishi kumfurahisha yeye, yani Magugi ni mungu huko Muifufu”....
alielezea bwana yule ambaye nilikuwa nikijua sasa kuwa
alikuwa akiitwa Mnaro.
“Bwana wewe kwani uko wapi na kwanini
hatukuoni?” baba yangu naye alipata swali la kuuliza na
akajibiwa..
“Niko mbali sana na hapo mlipo, ingawa naweza kuwaona na
kuituma sauti
yangu mpaka hapo mlipo” iliongea sauti ile nami nikapata
shauku ya kujua jambo nikauliza “unaweza kuona na kupeleka sauti mpaka Muifufu?”
nikajibiwa “ndio ninao uwezo huo ingawa huwa naishia
kuangalia nini kinaendelea huko Muifufu lakini huwa situmi sauti kwamaana huwa
sitaki baba yangu ajue kama huwa naona kinachoendelea huko na kwa kutuma sauti
atajua mara moja. “tafadhali niangalizie kama mke wangu yuko salama huko”
nilijikuta nimetoa ombi na sauti ikanijibu
“nadhani ingekuwa bora uangalie na umuone mwenyewe”.....
“Nitashukuru sana kama utanisaidia kwa hilo” nilijibu huku
sauti yangu ikionyesha waziwazi kiherehere cha kutaka jambo hilo litokee
haraka. “kifaa kinachoniwezesha kutekeleza jambo hilo kiko hapa kwangu na
hakiwezi kutoka hapa, itakubidi uje huku ili uweze kuona” ilielezea sauti ya
mzee yule nami nikamjibu “haina shida mzee, nielekeze nije sasa hivi” ...
“huwezi kufika kwangu mpaka mimi nikulete, nitakuja kukuchukua usiku kama kweli
uko tayari” ilisema ile sauti nami nikakerwa kidogo na tabia ile ya kutaka kila
jambo lichelewe kutendwa, nikajikuta nimeuliza kwa mara nyingine “kwani hauwezi
kuja kunichukua asubuhi hii nikaja huko?” sauti ile ikatulia kwa muda kisha
ikanijibu “kua mchawi kunataka subira, kuna mambo mengi ya kuyafanya kwa upole
na ukiwa na haraka kama hii yako utajikuta umepoteza kila kitu, kama kweli
unataka kuwa mchawi jifunze hilo” hapo nikakumbuka tena kuwa napaswa kua
mchawi, jambo ambalo hata sijui litafanikishwaje. “kwanini ni lazima awe mchawi
ila kutekeleza haya majukumu?” safari hii ni baba ambaye aliuliza.. “kwa sababu
bila ya kua mchawi hatoweza kufanya chochote ndani ya Muifufu, atakuwa anajipeleka
kuuawa tu. Ili kufanikiwa anapaswa kuwa mchawi, tena mchawi hasa ili aweze
kushindana na wachawi wa huko wenye uwezo mkubwa mno” baba akauliza tena “ wewe
ni mchawi tayari, kwanini usitusaidie tu mara moja kwa hili?” sauti ile
ikajibu, tena ilionesha kukasirshwa kama sio kuchoshwa na maswali yale.. “naona
kama tunarudi nyuma kila baada ya kupiga hatua moja, kua mchawi sio jambo kubwa
kama ambavyo ninyi mnaliona! Ni swala la kujua tu mbinu na kuzitumia, sio
lazima uanze kuua au kuwangia watu, kila mtu anaamua jinsi ya kuutumia ujuzi
anaoupata!. Ndio maana nikasema nakuachia siku nzima ya leo kisha kesho
utafanya maamuzi” sauti ile ilitulia nasi tukawa kimya, baadae nikavunja ukimya
“mimi niko tayari mzee, wala haina haja ya kungoja kesho ili nifanye maamuzi”
sauti ile ikacheka kisa ikasema “tumerudi nyuma tena, jifunze kuwa na subira
kama kweli unataka kuwa mchawi, tutaonana usiku” kisha kimya kikatawala.
Tulibaki pale tukiwa tumeduwaa, hakuna ambaye alikuwa
akiongea! Nadhani kila mmoja alikuwa akijaribu kuwaza na kuwazua kama ambavyo
nilikuwa nikifanya mimi. “Bado mna mpango wa kwenda kwa mganga?” mzee Miale
alivunja ukimya na mimi nikamuangalia baba kama ishara ya kumtupia yeye swali
hilo ili afanye maamuzi baada ya ambacho tumekiona.. “tujifunze kuwa na subira”
alijibu baba akiigiza ile sauti tukacheka kisha tukaaga na kuondoka.
Usiku wa siku hiyo tulikuwepo nyumbani mapema, tukala na
kuingia vyumbani mwetu! Yalikuwa kama majira ya saa tatu na sikuwa na usingizi
hata kidogo, nilikuwa na hofu kidogo huku nikimgoja mzee yule nikiwa sina
uhakika kama atakuja ama laa!..
Sijui hata saa ngapi nilipitiwa na usingizi ila nilikuja
kujikuta nikiisikia sauti ya mtu ikiniita kwa mbali kama naota vile,
niliposhituka nilijikuta katika mzingira ambayo sikuwa nikiyajua. Mbele yangu
alikuwa amesimama mtu ambaye sikuwa nimewahi kumuona! Alikuwa ni mwanume wa
makamo tu, hakuwa mzee wala hakuwa kijana. “karibu bwana, hapa ndipo ambapo
napatikana” aliongea bwana yule lakini ilikuwa ni sauti ile ambayo
ilitutembelea kwa mzee Miale na hata ambayo alikuja nayo mzee aliyenifuata
nyumbani! “wewe ni Mnaro?” niliuliza baada ya kuhisi kuwa alikuwa yeye “ndio”
alijibu kwa kifupi nami nikashangaa kwa maana sio yeye ambaye alikuja kwangu
usiku ule. “na yule mzee ambaye alikuja kwangu alikuwa nani?” niliuliza naye
akanijibu huku akiwa ameshughulika kufanya shughuli ambazo hazikueleweka,
alikuwa akihamisha hamisha vitu kama vile ambaye alikuwa akikipanga upya chumba
kile ambacho kilijaa makorokoro.. “nilikuwa ni mimi pia” akawa amenichanganya
lakini akaendelea na kunipa mwanga “ninao uwezo wa kuonekana kama kijana, kama
mzee, kama mtoto, kama mwanamke au hata kama mnyama yoyote yule” sasa alikuwa
amesogeza mbele yangu kitu kama beseni kubwa sana ambalo lilikuwa
limetengenezwa kwa matirio kama ya mbao hivi, kuangalia ndani ya beseni lile
kulikuwa kuna kimiminika cha rangi nyekundu. “sasa ni wakati wa kumuona mkeo”
aliongea mzee yule nami nikayalengesha macho yangu zaidi ndani ya beseni lile
lakini hakukuwa na chochote ambacho kilionekana! Lakini akaanza kunyunyizia
ungaunga ambao ulikuwa ukionekana kama majivu kisha akachukua kipande cha
kitambaa na kuanza kukisemea maneno kisha akanikabidhi, nilipokiangalia vizuri
niligundua kuwa kilikuwa kipande cha nguo ambayo aliivaa mke wangu siku ile ambayo
alipotea, nikashangaa nguo ile aliipata wapi mzee yule kwa maana nilijua kua
nguo ile ilikuwa nyumbani. “ili kumuona mtu hapa unatakiwa kuweka humo nguo
yake ambayo aliivaa na haijafuliwa, ukitaka kumuona mkeo weka humo kipande
hicho cha nguo yake” alisema yule mzee nami nikauliza “lakini mbona nguo yake
iko nyumbani?” yule mzee akaniangalia kisha akaniuliza baadala ya kunijibu
“kwani wewe ulikuwepo hapa? Haukuwa nyumbani?” nikabaki bila jibu wala swali
lingine la kuuliza kisha nikawa nakiingiza kitambaa kile ndani ya kimimkinika
kile ambacho nilianza kudhani kuwa kilikuwa damu. Mara niliona kimiminika kile
kikianza kuchemka polepole, huku kikiongeza kasi ya kuchemka kadri muda
ulivyozidi kwenda na mara kikaanza kuzunguka ndani ya beseni lile kubwa la mbao
kisha nikaona kama macho yangu yanavutwa ndani ya beseni lile nikawa najaribu
kujivuta kurudi nyuma lakini sikuweza kushindana na nguvu ile nikajiona kama
ambaye napoteza fahamu!......
Akili iliporudi sawa
nikajikuta nimesimama katika mazingira ambayo sikuwa nikiyajua,
Huo ni utangulizi tu
Kupata full …
Whatsapp +255 758 018 597
Email – kulayagroup@gmail.com
0 Comments
Karibu sana, tuma ujumbe whatsapp +255 758 018 597 kujipatia simulizi zetu
Emoji